Sakata lililoshika hatamu katika kipindi kifupi cha
nyuma ni kuhusu mshambuliaji wa Yanga, Emmanuel Okwi aliyedaiwa kuwa na usajili
wa utata na kusababisha Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kumsimamisha mpaka lipate
ufafanuzi kutoka Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).
Mchezaji huyo raia wa Uganda, alisajiliwa na Etoile du
Sahel ya Tunisia akitokea Simba Januari, 2013 kwa mali kauli ya dola 300,000
(Sh milioni 480) ambazo hazijalipwa mpaka sasa, kisha akashindwana na timu hiyo
akarejea kwenye timu yake ya awali, SC Villa ya Uganda kwa makubaliano maalum
na baadaye akatua Yanga, usajili uliozua utata mkubwa nchini.
Pamoja na sarakasi zote hizo zilizotokea lakini wiki
iliyopita tamko rasmi lilitolewa na TFF kwamba Okwi ni mchezaji halali wa Yanga
baada ya kupokea ufafanuzi waliokuwa wakiuhitaji kutoka Fifa.
Pamoja na ruksa hiyo, bado kuna maswali yanayohitaji
majibu ambapo Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa, amefafanua kila kitu:
Villa ilipata vipi uhalali wa kumuuza Okwi wakati alikuwa
akicheza hapo kwa makubaliano maalum?
“Okwi hakuwa kwa mkopo Villa wala kwa makubaliano
mengine, bali alipokuwa na matatizo na Etoile ambayo yalifika Fifa ndiyo kuna jaji
mmoja kutoka Fifa alitoa hukumu kwamba Okwi arudi Villa na ITC yake pia
wakakabidhiwe Villa, kwa hiyo timu inapokuwa na ITC ya mchezaji, ndiyo inakuwa
na mamlaka yote juu yake.”
Je, Yanga ilimsajili kama mchezaji huru?
“Okwi hakuwa mchezaji huru, alinunuliwa kutoka Villa,
Villa walimuuza kwa vigezo vyote kwenda Yanga.”
Kanuni gani iliyoufanya mkataba wake Etoile kuvunjwa?
“Tulipolifikisha hili suala Fifa sisi tulitaka kujua tu
kama Okwi ni halali kucheza Yanga ama la, hatukutaka ufafanuzi mrefu sana.
“Kikubwa ni kujua kama anaweza kucheza Yanga kutokana
na usajili wake ulivyokuwa una maswali mengi kwa sababu Simba pia walitufuata
na kutaka kujua nini kimetokea kwa Okwi mpaka katua Yanga, kwani hata wao pia
walikuwa na kesi yao inayoendelea kule kuhusu mchezaji huyohuyo na inayohusu
pesa za usajili wake.
“Kitu cha msingi ni kwamba Fifa wametuambia anaweza
kucheza Yanga, kuhusiana na kanuni ipi ilitumika kuvunja mkataba wake na
Etoile, hiyo siyo juu yetu.”
Mbona suala la Okwi kuruhusiwa Yanga limewahi
kumalizika huko Fifa kuliko lile la madai ya Simba kwa Etoile?
“Ilikuwa lazima liishe kwa haraka kwa sababu suala la
Yanga kuhusu Okwi lilikuwa linahitaji ufafanuzi tu na si vingine, kwa hiyo
ilikuwa ni ishu ya mtu au ofisa mmoja wa Fifa kukusanya data za Okwi kuangalia
mtiririko wake na kugundua uhalali uko wapi.
“Lakini kuhusu deni la Simba wanaloidai Etoile, ni
lazima lichukue muda kidogo kwa sababu ni madeni yale na ile ni kesi
inayoendelea, kuna utofauti kati ya kesi na ufafanuzi.”
Kwa hiyo suala la Okwi limekwisha kabisa au wanaendelea
kulifuatilia taratibu?
“Kikubwa kilikuwa ni kuhusu uhalali wake wa kuitumikia
Yanga, vyama pia vya nchi husika vilitakiwa kufahamu kuhusu hilo kwa kuwa
ndivyo pia vinavyohusika kumpitisha mchezaji kuchezea timu aliyosajiliwa kwa
kufuatilia taratibu zote, kwa hiyo majibu sasa yametolewa na yako wazi kuhusu
Okwi.”
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu wa Yanga, Benno
Njovu, amesema leseni ya kimataifa ya Okwi itakayomruhusu kucheza Ligi ya
Mabingwa Afrika kuanzia mchezo dhidi ya Al Ahly, inatarajiwa kufika kati ya leo
au kesho.
SOURCE: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment