KADUGUDA |
Kwa mara ya kwanza aliyekuwa Katibu Mkuu wa Simba, Mwina
Kaduguda, amefunguka kuwa, mwenyekiti wa klabu hiyo, Ismail Aden Rage, aliwahi
kumpa cheo cha ukatibu mara nne lakini akakataa.
Kaduguda aliyekuwa katibu wa Simba chini ya mwenyekiti
Hassan Dalali, amesema Rage alikuwa akimhitaji awe katibu mara nne katika
kipindi hiki cha karibuni lakini alikataa kwa kuhofia kuchafua CV
aliyoitengeneza Simba miaka ya nyuma kutokana na tofauti baina ya viongozi
waliopo sasa madarakani klabuni hapo.
Kaduguda alisema Rage alikuwa akiwasiliana naye mara
kwa mara kuwa anamhitaji kwa ajili ya utendaji na kurekebisha baadhi ya mambo
Simba lakini kwake akaona si sahihi kuwepo hapo kwa muda huu ambao Simba
imekuwa ikikumbwa na migogoro ya mara kwa mara.
“Rage aliniita mara nne katika kipindi hiki cha nyuma
walichokuwa wanatafuta katibu mkuu mpya na mara ya mwisho ilikuwa mwezi
uliopita lakini nikagoma kwa kuwa niliona kabisa kufanya kazi na uongozi uliopo
sasa ni kuchafua CV niliyokuwa nayo miaka ya nyuma Simba.
“Hata hivyo iweje aniite sasa wakati ni miaka minne
imepita tangu akae madarakani na hajawahi hata kunipigia simu kuniomba ushauri?
“Mwenyekiti hapatani na wajumbe wake wa kamati ya
utendaji, hii ni hatari na unaona ni jinsi gani ningeweza kwenda kuvunja
heshima yangu niliyoijenga wakati nipo na Dalali.
“Najua Simba wananihitaji lakini naweza nikaenda baada
ya uchaguzi huu kupita au nikagombea kwenye uchaguzi huu unaokuja kama nikitaka
lakini vinginevyo naweza nikabaki kuwa mwanachama muadilifu wa Simba,” alisema
Kaduguda.
SOURCE: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment