Kiungo Mtanzania, Mwinyi Kazimoto huenda
akaweka rekodi kucheza Ligi Kuu Qatar iwapo timu yake itashinda mechi tatu
zilizobaki.
Kazimoto anakipiga katika timu ya Al
Markhiya inayoshiriki Ligi Daraja la Pili nchini Qatar na sasa katika nafasi ya
nne katika msimamo wa ligi hiyo.
Al Markhiya ina pointi 21 katika nafasi
hiyo ya na iwapo itashinda mechi zake tatu zilizobaki basi itakuwa na uhakika
wa kupanda ligi kubwa zaidi nchini humo.
![]() |
| KAZIMOTO AKIWA NA KIKOSI CHA AL MARKHIYA |
Akizungumza kutoka Doha, Qatar, Kazimoto
alisema wana hamu ya kupanda daraja na wamekuwa wakijitahidi kucheza kwa
kujituma hadi walipofikia hapo wakiwa na mechi tatu.
“Ligi ni ngumu sana kwa kweli, kuna
ushindani wa hali ya juu kuliko watu wanavyotegemea. Unajua timu za hapa zina
uwezo kifedha hivyo zinasajili wachezaji kutoka Ulaya, mfano Hispania, Ureno na
pia hata kutoka Brazil, Argentina, Chile na kwingine.
“Hali hiyo inasababisha kuwe na
ushindani kuwa mkali sana, lakini tutajitahidi kadiri ya uwezo wetu na kama
tukishinda mechi hizo tatu mambo yatakuwa uhakika,” alisema akionyesha
kujiamini.
Kazimoto sasa amekuwa akiaminika katika
kikosi hicho na ndiye amepewa ‘dimba la juu’ yaani namba nane na jukumu lake
kubwa ni kuichezesha timu hiyo ambayo imekuwa na mabadiliko makubwa msimu huu.
Kiungo huyo aliyeanza kuchipukia akiwa
na Ruvu Shooting, alijiunga na Al Markhiya akitokea Simba iliyoona kipaji chake
na kumsajili na baada ya hapo aliendelea kufanya vizuri hadi alipojiunga na
timu hiyo ya Qatar.









0 COMMENTS:
Post a Comment