![]() |
| MASHABIKI WA MBEYA CITY KWENYE UWANJA WA SOKOINE, TAYARI KUIUNGA MKONO TIMU YAO. MWANZA HAWANA TIMU YA KUIUNGA MKONO NA WENGI WAMEKALIA MAJUNGU NA KUTOPENDANA? |
ENZI zile za Pamba ya Mwanza ambayo
ilipewa majina lukuki yakiwemo kama TP Lindanda, Wana Kawekamo na mengine mengi
ambayo yalitokana na ubora wa kikosi cha timu hiyo.
Pamba ya Mwanza iliundwa na wachezaji
wengi mahiri ambao walipokutana na timu nyingine iwe Yanga, Simba, Majimaji,
Coastal Union, African Sports, Sigara, Pilsner, Nyota Nyekundu au nyinginezo,
basi habari walikuwa wanaipata.
Soka wakati huo, kila timu ilikuwa na
wachezaji wake nyota, nakukumbusha Majimaji yenye watu kama Celestine Sikinde
‘Mbunga’, Coastal Union yenye akina Razak Yusuf ‘Careca’, Kasa Mussa, Juma
Mgunda na Wenzao, Reli Morogoro na watu kama Mbuyi Yondani na David Mihambo walivyokuwa
na uwezo mkubwa, lakini bado Pamba ya Mwanza iliendelea kung’ara na kufanya
vizuri.
Mara nyingi siku hizi, wanamichezo wengi
katika mikoa wanasema wanasema wanashindwa kuwa na timu imara kwa kuwa enzi
hizo walikuwa wakisaidiwa sana na mashirika kuziendesha timu, wachezaji
walikuwa wakilipwa mishahara na baada ya hapo, mambo yamekuwa magumu.
Leo si lahisi tena kwa Mwanza kuwasikia
wachezaji wenye sifa kama Fumo Felician, Kitwana Selemani, Mao Mkami ‘Ball
Dancer’, George Masatu, Hussein Amani Masha, Khalfan Ngassa, Rajab Rashid na
wengine wengi kwa kuwa tu, hakuna mipango tena.
Kweli hakuna mashirika ambayo yanakubali
kuziongoza timu, kwa kuwa ni hivyo, pamoja na mkoa Mwanza kuwa na vipaji lukuki
ambavyo vinaendesha karibu asilimia 50 ya timu za soka zinazofanya vizuri,
wadau wake wamelala na huenda wanasubiri tena mashirika yaanze ili kujengwa kwa
Pamba upya.
Mwanza ni mmoja wa mkoa unaoongoza kwa
kuwa na wachezaji wakongwe waliowahi kung’ara katika soka, lakini leo hawana
ushawishi wowote, wengi wamekalia majungu, wamejitenga na kuwa mamluki wa timu
za Dar es Salaam huku wakiuacha mkoa wao maarufu kwa soka ukibaki hauna hata
timu ligi kuu, aibu na kichekesho lakini ajabu hakuna anayeona aibu.
Wakati Toto African ikiwa Ligi Kuu
Tanzania Bara, asilimia kubwa ya wakongwe wa Mwanza wenye mapenzi na Simba kwa
kushirikiana na wadau wengine waliona bora iteremke daraja kwa kuwa ina asili
ya Yanga. Lakini wako ambao wanashabikia Yanga, hawakutaka wenzao wenye mapenzi
na Simba waingie na kuisaidia kwa madai si damu yao.
Sasa wote wamekaa hawana lolote
wanalolifanya zaidi ya kucheza Ma-bonanza na ndiyo umekuwa umaarufu wa Mwanza
wakati mkoa kama Mbeya sasa umefikisha timu mbili huku watu wake wakiendelea
kuungana bila ya kutegemea kampuni yoyote.
Kama Mbeya City inasaidiwa na Manispaa
ya Mbeya na sasa ndiyo timu kutoka mkoani, yaani nje ya Dar es Salaam
inayofanya vizuri kuliko nyingine yoyote, vipi Mwanza ambalo ni jiji kubwa
kuliko Mbeya na lenye vipaji lukuki vya soka lishindwe? Hiki ni kichekesho na
ajabu wanasoka na wadau wa mchezo huo wamejazana Mwanza, wakiwa katika usingizi
wa pono, hakuna anayejua na wanaabudu majungu.
Kweli kama ulifanikiwa wakati unacheza
soka, ukaogelea sifa lukuki ambazo umezeeka nazo, halafu wakati huu unaogelea
katika dimbwi la waliofeli kuhamasisha mafanikio ya mchezo uliofanikiwa, una
haja gani ya kuitwa gwiji? Wakongwe wa Mwanza wenye majina makubwa wako wapi,
nini kinawakwamisha na kama wao wana nia na wanakwamishwa, nani amefungua
mdomo?
Au wanaridhika na umamluki wa kuona timu
za Dar es Salaam zikifanya vibaya na wao kushangilia kwa njia ya redio na
vyombo vya habari wakiamini inawatosha. Au hawaoni ni sahihi vijana kutamba
hapo Mwanza kwa kuwa wanaweza kufuta walichokifanya wao kwa kupata sifa zaidi?
Mimi nawaona ni watu wasio na mapenzi na mkoa wao, wasiojua umuhimu wa
wanapoishi na badala yake wanakubali kuwa vibaraka wa Dar es Salaam kwa kuwa tu
hawajui mapenzi ya dhati ya wanapoishi, yaani Mwanza.
Kama kukosea mmekosea sana, Mwanza
haistahili inachopata katika soka la Tanzania na wanaosababisha ni wadau
wakiwemo viongozi wa vyama vya soka na wakongwe lukuki waliojazana Mwanza
wanaoshabikia timu za Dar es Salaam. Sasa badilikeni, mnaweza kujifunza kwa
Mbeya wala msione haya hata kidogo.








0 COMMENTS:
Post a Comment