Mabingwa wa Tanzania Yanga watacheza
mechi yao ya marudiano na Al Ahly bila ya kuwa na mashabiki watakaoingia
kutazama mechi hiyo.
Mechi hiyo itakayopigwa Machi 8 au 9
jijini Cairo haitakuwa na mashabiki isipokuwa wachache tu watakaopata kibali
kutoka kwa Shirikisho la Soka la Misri (EFA).
Mwaka juzi zilizuka vurugu kubwa baada
ya timu ya Al Masry kuwachapa vigogo Al Ahly kwa mabao 3-1, hali iliyosababisha
watu 74 kupoteza maisha na wengine 1,000 kujeruhiwa wakiwemo wengine
waliojeruhiwa vibaya sana. Baada ya hapo, mechi zinachezwa nchini humo,
mashabiki wamekuwa hawaruhusiwi.
Mmoja wa maofisa wa EFA
aliyejitambulisha kwa jina la Amir Mohammed aliliambia Championi Ijumaa juzi
kuwa hakuna mashabiki watakaoruhusiwa kuingia uwanjani wakati wa mechi hiyo ya
Ligi ya Mabingwa Afrika kutokana na sababu za kiusalama.
“Kawaida hata katika mechi za ligi watu
wachache wenye kibali maalum wamekuwa wakiingia uwanjani, hakuna
atakayeruhusiwa kuingia. Hivyo kama itakuwa ni Ahly na timu ya Tanzania,
hakutakuwa na mashabiki.
“Labda wachache sana ambao tutawapa
kibali, lakini kawaida ni viongozi na waandishi wa habari pekee. Zaidi ya hapo
hatuwezi kuruhusu watu, waambie Yanga wanapaswa kulijua hilo,” alisema.
Ili kupata uhakika, gazeti hili liliamua
kuwasiliana na baadhi ya Watanzania wanaoishi katika jiji la Cairo na mmoja wao
aitwaye Mohamed Mdoe alisema kawaida mashabiki katika jiji hilo wamekuwa
wakiangalia mechi za ligi kuu kupitia runinga.
“Hakuna anayekwenda uwanjani, unajua
baada ya zile vurugu za mashabiki hadi watu wakafariki dunia, walifungiwa na
tumeishazoea. Mechi tunaziangalia kupitia runinga tu hapa,” alisema Mdoe.
Kawaida mashabiki husafiri na timu
zinapokwenda kucheza na wengi wa Yanga wangependa kwenda na timu yao jambo
ambalo sasa linaonekana litakuwa gumu kutokana na adhabu hiyo wanayoitumikia
Misri kutokana na vurugu hizo zilizosababisha hadi watu kupoteza maisha.








0 COMMENTS:
Post a Comment