Na Saleh
Ally
MAKOCHA wageni
waliojiunga na Simba na Yanga kwa ajili ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara
kuanza sasa wanaweza wakawa wameanza kupata picha kamili ya kazi yao.
Yanga na
Simba, kila moja inataka kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara, hakuna ubishi kama
itashindikana kila moja inaona afadhali kubaki katika nafasi ya pili.
Nafasi ya
pili inatoa nafasi kwa timu hizo kushiriki Kombe la Shirikisho ambayo pia ipo
chini ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf) kama ilivyo kwa Ligi ya Mabingwa
Afrika.
Lakini
nafasi hizo mbili zimegeuka na kuwa lulu, tayari timu nne zimeonyesha kuwa na
nguvu sana katika kuziwania, Yanga, Azam FC, Simba na Mbeya City. Si rahisi kwa
sasa kusema moja kati ya hizo tayari imefanikiwa.
Lakini bado
kuna washindani ambao hawapaswi kudharauliwa sana, kwamba hata kama
wasipopata kati ya nafasi hizo, wanaweza
kuwa tatizo kwa wanaowania. Mfano Coastal Union na Mtibwa Sugar, viko vizuri.
Kocha
Zradvko Logarusic wa Simba na Hans van Der Pluijm wa Yanga ambao wote wameanza
kazi kamili kwenye mzunguko wa pili, kila mmoja sasa anaweza kuwa ameona njia
sahihi anayotakiwa kupita na huenda ni wakati mwafaka wa kuamini ligi hiyo
haitabiriki.
Inawezekana
makocha wote waliichukulia ligi hiyo kama ‘poa’ fulani hivi. Lakini mechi zao
tatu za mwanzo, tayari wameona tofauti kubwa ambayo ndiyo picha halisi ya ligi
hiyo kwamba si ya mzaha.
Wote wawili
wamewahi kufanya kazi nchini Ghana, lakini Logarusic akajikita Kenya akiwa na
Gor Mahia, bado wana kila sababu ya kujifunza kwenye Ligi Kuu Bara, kwamba si
lelemama.
Wote wawili
katika mechi zao tatu za mwanzo walipoteza pointi mbili na kuchanga saba. Maana
yake Yanga na Simba, zilishinda mechi mbili na kutoa sare moja.
Yanga
ilianza na ushindi wa bao 2-1 dhidi ya Ashanti United, ikatoka sare ya bila
kufungana na Coastal Union na mechi ya tatu ikaifunga Mbeya City bao 1-0 ikiwa
ni mara ya kwanza kwa timu hiyo ya Mbeya kupoteza mchezo.
Simba
ilianza na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Rhino, ikaendeleza ushindi kwa kuifunga
Oljoro mabao 4-0 halafu ikapunguzwa kasi ya bao 1-1 dhidi ya Mtibwa Sugar.
Kila timu
imeacha pointi mbili ndani ya mechi tatu, kwani zingeshinda zote kila moja ingepata
pointi tisa, lakini kila sare imedondosha pointi mbili.
Kingine
kinachovutia, makocha hao wawili wameonyesha kuteswa na mechi za ugenini, kwani
Yanga ilipotoka kwa mara ya kwanza ikakutana na sare ‘tasa’ dhidi ya Coastal
Union mjini Tanga na Simba ikaenda mwendo huo kwa sare ya 1-1 dhidi ya Mtibwa
Sugar mjini Morogoro.
Simba
imecheza mechi ya nne kabla ya Yanga, tayari Logarusic ameonja ladha ya kipigo
katika Ligi Kuu Bara baada ya kuchapwa na Mgambo JKT kwa bao 1-0 kwenye Uwanja
wa Mkwakwani, Tanga. Yanga bado hawajacheza mechi ya nne, inafuatia Februari 19
dhidi ya Azam FC, itakuwa big match.
Si
Logarusic wala van Der Pluijm ambaye amewahi kushinda mechi ya nje ya Dar es
Salaam ingawa mmoja amecheza mbili na mwingine moja.
Pamoja na
uzoefu wa makocha hao kwa kuwa wamewahi kufanya kazi ya ukocha katika nchi
zaidi ya mbili, lakini kazi ya soka ya Tanzania wamegundua si rahisi na kuna
timu ambazo hazijatumia gharama kubwa kwenye usajili, lakini zina uwezo mkubwa.
Mfano mzuri
mabadiliko ya Mgambo JKT ambayo mzunguko wa kwanza ilipigwa na Simba mabao 6-0,
lakini mzunguko wa pili imejibu na kubeba pointi zote tatu kwa kuishinda Simba
bao 1-0.
Wakati
makocha hao wawili wanalazimika kuzungumza kwa rekodi, ugumu unazidi kuongezeka
kuwania ubingwa au hata nafasi ya pili kwa kuwa Mbeya City ambayo ilipoteza kwa
mara ya kwanza dhidi ya Yanga, imeamka tena na kuichapa Mtibwa Sugar kwa mabao
2-1.
Mbio
zinaendelea, Azam FC pia ni washindani wakubwa, Mbeya City bado ina pumzi ya
kutosha. Maana yake, hakuna kulala kwa van Der Pluijm na Logarusic na kwao ligi
ni sawa na kama ndiyo imeanza vile kwa kuwa kwa kipindi hiki, rekodi ndiyo
zinazozungumza.
REKODI:
Logarusic
NYUMBANI
Cheza 2
Shinda 2
UGENINI
Cheza 2,
sare 1, poteza 1
Van Der
Pluijm
NYUMBANI
Cheza 2 Shinda
2
UGENINI
Cheza 1,
sare 1
SOURCE: CHAMPIONI







0 COMMENTS:
Post a Comment