February 19, 2014


Na Saleh Ally
KWELI ni mwaka wa tabu kwa Manchester United, wakati inaonekana kuwa imetoka katika mbio za kuwania ubingwa England, kwenye mbio za wanaowania uchezaji bora katika viwango vya uchezaji wa Premiership, pia hawana nafasi.


Kampuni ya EA Sports ambayo inadhamini Ligi Kuu England, hufanya kazi ya kutengeneza takwimu za ubora wa wachezaji kwa maana ya uchezaji kuanzia dakika, mchango kwa timu na alama wanazostahili kupata kutokana na ubora.
Katika wachezaji 10 walio na pointi nyingi hadi sasa za kuibuka kuwa kati ya wafungaji bora kwenye Ligi Kuu England, Rooney pekee na anashika nafasi ya tisa, huku Robin van Persie ambaye mwaka jana na juzi alishinda kwa ubora wa viwango kama ilivyokuwa mwaka juzi, hayumo hata kwenye 10 bora.
Van Persie ambaye alikuwa mfungaji bora pia alishika nafasi mbili za juu kwa ubora, hata baada ya Gareth Bale kutangazwa kuwa mchezaji bora wengi hawakukubaliana na hilo na kweli katika viwango vya EA Sports Mholanzi huyo alikuwa akiongoza.
Lakini msimu huu yuko nje ya 10 Bora, hali inayoonyesha kuwa kweli huu si mwaka wa Manchester United ambayo tokea David ‘Daudi’ Moyes achukue nafasi ya Alex Ferguson. Hii si habari njema kwa kikosi hicho cha ‘Mashetani Wekundu’.
Wachezaji 10 wanaowania kwa karibu tuzo ya viwango bora katika Ligi Kuu England ni Luis Suarez wa Liverpool, Eden hazard (Chelsea), Sergio Aguero (Man City), Steven Gerrard (Liverpool),  Yaya Toure (Man City), Daniel Sturridge (Liverpool), Mesut Ozil (Arsenal), Adam Lallana (Southampton), Wayne Rooney (Man United) na Aaron Ramsey (Arsenal).
Ukiachana na ishu ya Manchester kuonyesha kwamba haikuwa vizuri kwa viwango kwa kuwa haina wachezaji wengi kwenye 10 bora ya viwango bora kama ilivyozoeleka, lakini angalia ugumu wa ligi hiyo unavyoweza kufafanuliwa na watu hao 10 tu.
Watu hao 10 wamecheza jumla ya dakika 19,290 ikiwa ni sawa na saa 322 au siku 13. Maana yake kama utajumlisha dakika zao zote, watu hao wamekuwa uwanjani kwa siku zote hizo, si kitu rahisi, mwili unatakiwa kuwa fiti kweli. Hapa unaangalia nguvu na ushindani ndani ya ligi hiyo, kwamba si lelemama na muda wa kupumzika ni mdogo.
Kama wachezaji 10 tu, wanaweza kuwa wamecheza dakika zote hizo na msimu haujaisha, vipi kama utachukua wachezaji wote katika ligi hiyo, utapata dakika au siku ngapi?
Ni ligi ngumu ambayo inahitaji kujituma na kwa dakika hizo, utagundua kwa wachezaji wanaofanya vizuri wanaweza wakawa wamecheza mara tatu zaidi ya hapo kwa kuwa wanajikuta wanashiriki na ligi nyingine kama Kombe la Capital One na lile la FA.
Kwa mchezaji anayeweza kushiriki mara mbili ya dakika alizocheza si kitu rahisi, kinahitaji moyo wa kujituma, moyo wa kutaka ushindi, lakini anayefanya hivyo lazima awe fiti kweli kwa kuwa analazimika kukimbia muda mwingi sana uwanjani ili kufanya vizuri na kutoa majibu ya viwango vya juu.
Katika hiyo 10 bora, anaongoza Suarez ambaye amecheza mechi 21, kati ya hizo amepiga dakika 1884 akiwa amepewa pointi 867, zinazomfanya kuwa kileleni kati ya wachezaji wanaopewa nafasi ya juu ya viwango. Msimu uliopita alishika nafasi ya pili baada ya kupitwa na van Persie katika mechi za mwisho kwa kuwa alifungiwa kutokana na kumng’ata mkononi beki Blanislav Ivanovic wa Chelsea.
Nafasi ya pili ni Hazard, amecheza mechi 26, akiwa amepiga jumla ya dakika 2190 na amekomba pointi 691, mkali Aguero yuko katika nafasi ya tatu katika mechi 17 alizocheza, akiwa na dakika 1199 na pointi 553.
Nafasi ya nne na tano inakwenda kwa viungo akianza Gerrard aliyecheza dakika mechi 22 kwa jumla ya dakika 1843, amepata pointi 553 na Yaya Toure aliyekipiga katika mechi 24 na ana dakika 2092 na jumla ya pointi 546.
Wengine watano walio katika 10 bora ni Sturridge (amecheza mechi 18, dakika 1417 na pointi 527), Ozil (amecheza mechi 21, dakika 1810 ana pointi 527), Lallana (amepiga mechi 26, dakika 2109 na amechukua pointi 511).
Wawili wa mwisho wanaofunga 10 bora ni Rooney (amecheza mechi 21, dakika 1756 na ana jumla ya pointi 503) na Ramsey (amekipiga mechi 18, dakika 1495, amekusanya jumla ya pointi 95).




0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic