Na Saleh Ally
WIKI iliyopita kulikuwa na mechi zaidi ya tano za Ligi Kuu
England na mashabiki wa soka duniani kote walivutiwa zaidi na mechi kati ya
Arsenal na Manchester United inayoongozwa na David ‘Daudi’ Moyes.
Mechi hiyo iliwavuta wengi wakiwemo mashabiki wa soka nchini
kwa kuwa Arsenal inafanya vizuri, inagombea ubingwa wa ligi wakati Man United
imekuwa ikisuasua, si kama ile iliyokuwa chini ya Alex Chapman Ferguson.
Mashabiki walitaka kujua kama kweli Manchester ya Moyes
ingeweza kupambana na Arsenal ya Arsene Wenger ambayo inapambana vilivyo
kuhakikisha inatwaa ubingwa huku United ikionekana imeishatoka kwenye mbio hizo
licha ya kuwa mabingwa watetezi.
Kingine kilichowavutia wengi ni Arsenal kuwa na safu ngumu
ya ulinzi lakini soka la kuvutia zaidi ya Man United ambayo wakati wa Ferguson
ilikuwa ina sifa za kucheza kwa kasi na mara nyingi ilipokutana na Arsenal
ndiyo iliyoonyesha soka la kuvutia zaidi.
Mashabiki wengi walikaa kwenye runinga na kutaka kuona
kitakachotokea, kweli ilikuwa mechi nzuri iliyoonyesha ufundi wa juu, lakini
ikawaudhi wengi baada ya dakika 90, matokeo yalikuwa sare ya bila kufungana.
Wanasema raha ya mechi mabao, hivyo mashabiki kila upande
walitaka kuona mabao yanafungwa, nani angefunga, yupi alitoa pasi ya bao halafu
mwisho simulizi la mechi yenyewe lizidi kuwa juu.
Wakati mashabiki wakionekana kutofurahishwa na mechi hiyo
kwisha kwa sare ya bila kufungana, wataalamu ambao hufanya tathmini za
kitaalamu kutengeneza takwimu za kila mechi katika Ligi Kuu England, Kampuni ya
EA Sports, wao wakaipa cheo mechi hiyo.
Mechi kati ya Arsenal dhidi ya Man United ndiyo mechi bora
ya wiki hiyo kutokana na namna ilivyochezwa pamoja na kwamba hakukuwa na bao
hata moja lililofungwa katika dakika zote 90. Unaamini hilo?
Watalaamu hao wana vigezo vyao vya kitaalamu walivyovitoa
kuhusiana na mechi ilivyokuwa hadi kuwa bora, sehemu ya vigezo hivyo ni kasi ya
mchezo kwa mchezaji mmojammoja na mwendo wa kila timu, halafu wakachambua
wachezaji.
Wataalamu hao wanaeleza kwamba, mechi hiyo wachezaji
walikimbia zaidi kuliko mechi nyingine zote zilizochezwa wiki hiyo na jumla ya
wingi wa kilomita kwa kila timu kama ukijumlishwa, maana yake ndiyo mechi bora
na inaonyesha wachezaji walikuwa fiti zaidi.
Jumla ya kilomita walizokimbia wachezaji wote wa Manchester
United walioanza na kuingia ni 74.1 wakati wenyeji Arsenal wenyewe walipata
jumla ya kilomita 69.7 na kama zikijumlishwa ni kilomita 143.8.
Kilomita 143.8 kwa mechi moja ilikuwa juu zaidi ya nyingine
zilizochezwa, pia ni kigezo cha kuonyesha timu zote zilikuwa fiti na mechi
ilikuwa bora kwa kuwa kukimbia kwa umbali mrefu kunaonyesha hakukuwa na ujanja
wa kupoteza muda na kila timu ilicheza kiushindani zaidi.
Kwa wachezaji mmojammoja, pia Michael Carrick ambaye huenda
mashabiki wa Man United hawakuliona hilo, ndiye alikimbia kilomita 7.5 ambazo
ni nyingi zaidi ya wengi uwanjani na kufuatiwa na Mikel Arteta aliyekimbia 7.3.
Ukiachana na wingi wa kilomita, walikuwepo wachezaji waliokwenda
kasi zaidi ya wengine, hasa katika mipira ambayo walitanguliziwa au wale
waliokuwa wakikimbizana na mafowadi kwenda kuondosha hatari langoni mwao.
Alex Oxlade-Chamberlain aliyecheza dakika 16 tu akitokea
benchi, alikimbia kwa kasi ya kilomita 33.2 kwa saa na kuweka rekodi ya
aliyekimbia kasi ya juu zaidi katika mechi hiyo na wachezaji wengine wote
katika Premiership wiki hiyo iliyopita.
Alifuatiwa na beki Nemanja Vidic wa Man United ambaye
alikimbia hadi kufikia kilomita 33.1 na wengine walioonyesha wana kasi kubwa ni
Mesut Ozil (Arsenal) kilomita 32.9 na Chris Smalling, kilomita 32.4.
MAPAFU YA MBWA…
ARSENAL DAKIKA KM
Mikel Arteta 90 7.3
Santiago Cazorla
90 7.0
Mesut Ozil 90 7.0
Jack Wilshere 90 6.9
Olivier Giroud 90 6.7
JUMLA YA MWENDO KWA WACHEZAJI WOTE 69.7
MAN U DAKIKA KM
Michael Carrick
90 7.5
Wayne Rooney
90 7.4
Robin van Persie
90 7.0
Tom Cleverley
90 7.0
Chris Smalling 90 6.8
JUMLA YA MWENDO KWA WACHEZAJI WOTE 74.1
WENYE KASI KUBWA…WEN
ARSENAL DAKIKA KM/H
Oxlade-Chamberlain
16 33.2
Mesut Ozil 90 32.9
Olivier Giroud
90 32.6
Laurent Koscielny 90 31.3
Bacary Sagna 90 31.3 LaL
MAN U DAKIKA KM/H
Nemanja Vidic 90 33.1
Chris Smalling 90 32.4
Juan Mata 75 32.4
Rafael 45 32.4
Wayne Rooney 90 31.5
0 COMMENTS:
Post a Comment