Uongozi wa Klabu ya Simba umeweka wazi
kuwa suala la kumuongezea mkataba kocha wake mkuu wa sasa, Zdravko Logarusic limewekwa
pembeni kwa kuwa wanasubiri kuona mwelekeo wa timu yao ambayo imekuwa haina
matokeo mazuri hivi karibuni.
Loga raia wa Croatia alisaini mkataba
wa miezi sita wakati alipotua klabuni hapo mwishoni mwa mwaka jana, ambapo
mkataba huo unatarajiwa kufikia tamati Juni mosi, mwaka huu.
Katibu Mkuu wa Simba, Ezekiel Kamwaga, aliweka wazi kuwa matokeo ya timu katika
mechi zilizosalia ndiyo yatapa picha uongozi juu ya kuongeza au kutoongeza
mkataba huo.
“Mkataba wake unatarajiwa kufikia
tamati Juni mosi, mwaka huu tutaendelea naye mpaka mwisho wa ligi, makubaliano
yetu ya awali yalikuwa ni kumpa mkataba wa muda mfupi ili kumuangalia na iwapo
atafanya vizuri na kuridhisha basi tutamuongezea.
“Lakini suala hilo litaamuliwa mwisho
wa ligi kwa wanachama na viongozi kutathmini kile alichokifanya na kama kubaki
ama kutobaki ni maamuzi yatakayotolewa hapo baadaye,” alisema Kamwaga.
Simba inashika nafasi ya nne katika
msimamo wa Ligi Kuu Bara ambapo hivi karibuni iliambulia pointi mbili kati ya
12 ilizotakiwa kuzipata katika mechi nne za ligi hiyo.
0 COMMENTS:
Post a Comment