Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF) na Kocha wa Taifa Stars, Kim Poulsen wamekubaliana kuvunja mkataba katika
makubaliano ambayo ni siri kwa pande zote mbili.
Ingawa ni lugha ya kupoza mambo, lakini ukweli TFF imemfuta kazi kocha huyo na tayari iko katika mchakato wa mwisho kupata kocha mpya.
Uamuzi huo umetangazwa leo (Februari
27 mwaka huu) jijini Dar es Salaam kwa pamoja na Rais wa TFF, Jamal Malinzi na
Kocha Poulsen mbele ya waandishi wa habari.
Rais Malinzi kwa niaba ya TFF ametoa
shukrani za dhati kwa Kocha Poulsen kwa ushirikiano na mchango ambao ameutoa
kwa Tanzania kuanzia kwenye mpira wa miguu wa vijana.
Naye Kim amewashukuru Watanzania kwa
ushirikiano waliompatia kwa kipindi cha miaka mitatu alichokaa nchini kuanzia
Mei 2011 alipoteuliwa kuwa kocha wa timu za Taifa za vijana, na baadaye Taifa
Stars.
Akizungumzia benchi jipya la ufundi
la Taifa Stars, Rais Malinzi amesema linatarajiwa kutangazwa hivi karibuni
likiongozwa na kocha kutoka nje ya Tanzania.
Amesema kwa upande wa mechi dhidi ya
Namibia itakayochezwa Machi 5 mwaka huu jijini Windhoek, Stars itaongozwa na
Kaimu Mkurugenzi wa Ufundi, Salum Madadi akisaidiwa na kocha Hafidh Badru
kutoka Zanzibar.
Katika hatua nyingine, Kocha Madadi
amewaondoa wachezaji watano wa Yanga katika kikosi kilichotajwa awali ili
wapate fursa ya kuitumikia timu yao kwenye mechi mbili za Ligi ya Mabingwa
Afrika dhidi ya Al-Ahly ya Misri.
Wachezaji hao ni Athuman Idd, David
Luhende, Deogratius Munishi, Frank Domayo, Kelvin Yondani na Mrisho Ngasa. Pia
kipa Ivo Mapunda ameondolewa katika kikosi hicho baada ya kupata msiba.
Nafasi zao zimezibwa na wachezaji
Abdi Banda (Coastal Union), Himid Mao (Azam), Juma Luizio (Mtibwa Sugar), Said
Moradi (Azam) na Shabani Kado (Coastal Union).
Taifa Stars itaingia kambini
keshokutwa (Machi 1 mwaka huu) jioni kwenye hoteli ya Accomondia jijini Dar es
Salaam, na itaondoka Machi 3 mwaka huu alfajiri kwa ndege ya South African
Airways na kurejea nchini Machi 7 mwaka huu saa 8.15 mchana.
0 COMMENTS:
Post a Comment