Wakati Zambia (Shepolopolo) imewasili
leo mchana (Februari 27 mwaka huu), Twiga Stars imesema mazoezi yamewaingia barabara
tayari kwa mechi dhidi ya Wazambia hao itakayochezwa kesho (Februari 28 mwaka
huu).
Mechi hiyo ya marudiano ya raundi ya
kwanza ya michuano ya Afrika kwa Wanawake (AWC) itafanyika Uwanja wa Azam
Complex uliopo Chamazi kuanzia saa 10 kamili jioni, na hakutakuwa na kiingilio.
Wakizungumzia mechi hiyo, Kocha wa
Twiga Stars, Rogasian Kaijage na nahodha wa timu hiyo Sophia Mwasikili wamesema
kikosi chao kimewiva kwa ajili ya mpambano huo baada ya kufanyia kazi upungufu
uliojitokeza katika mechi ya kwanza.
Twiga Stars ilipoteza mechi ya kwanza
iliyochezwa Februari 14 mwaka huu jijini Lusaka kwa mabao 2-1, na inahitaji
ushindi ili iweze kusonga mbele kwenye michuano hiyo ambayo fainali zake
zitafanyika Oktoba mwaka huu nchini Namibia.
Iwapo Twiga Stars itafanikiwa kuitoa
Zambia katika mechi hiyo itakayooneshwa moja kwa moja na Azam Tv itacheza
raundi ya mwisho na Zimbabwe.
Msafara wa Shepolopolo una watu 26
ambapo wachezaji ni Anita Mulenga, Annie Kibanji, Carol Howes, Debora Chisanga,
Emelda Musonda, Esther Mukwasa, Grace Zulu, Hazel Nali, Hellen Mubanga, Lweendo
Chisamu, Meya Banda, Mirriam Katamanda, Misozi Zulu, Mupopo Kabange, Noria
Sosala, Rachel Lungu na Susan Banda.
Viongozi ni Maclean Daka, Charles
Bwale, Kaluba Kangwa, Enala Phiri, Cornelia Chazura, James Nyimbili, Besa
Chibwe, Dorothy Sampa na Kabungo Katongo.
0 COMMENTS:
Post a Comment