Waziri wa Habari, Utamaduni na
Michezo, Mhe. Dk. Fenella Mukangara anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye mbio
mbio za 12 za Kilimanjaro Marathon ambazo zinatarajiwa kufanyika Jumapili ijayo
tarehe 2 Machi, 2014 mjini Moshi.
Aggrey Marealle, Mkurugenzi Mkuu wa
Executive Solutions, waratibu wa mbio hizo alisema jana kwamba Dr. Mukangara
amekubali kuwa mgeni rasmi na atahuduria sherehe ya utoaji zawadi ambapo atatoa
zawadi kwa washindi kumi wa mbio defu za kilomita 42 maarufu kama Full Marathon
kwa wanaume na wanawake. “Uwepo wa waziri ni ishara ya uungaji mkono tukio hili
na ameeleza kufurahishwa kwake na maandalizi ya hali ya juu ya Kilimanjaro
Marathon. Dk. Mukangara ameeleza mara kadhaa kwamba serikali inaunga mkono
Kilimanjaro Marathon kwa kutambua mchango wake michezo, utalii na uchumi,”
alisema Marealle.
Marealle aliongeza kwamba baada ya
sherehe ya utoaji zawadi Waziri ataungana na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro na
mpenda michezo Mhe. Leonidas Gama, wawakilishi wa wadhamini na watu wengine
mashuhuri kwenye mlo maalum wa mchana uliodhaminiwa na Kibo
Palace Hotel. Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro binafsi na kupitia ofisi yake amekuwa
muungaji mkono wa Kilimanjaro Marathon na amekuwa akifurahia kukaribisha maelfu
ya watu wanaokuja Moshi kutoka mataifa mbalimbali.
John Addison, Mkurugenzi Mkuu wa Wild
Frontiers, waandaaji wa mbio hizo alisema “mbio za mwaka huu zimesheheeni
motisha mbalimbali za kuvutia ili kuongeza idadi ya washiriki. Washindi wa
kwanza kwenye mbio ndefu za kilomita 42 (Kilimanjaro Premium Lager Marathon)
wanawake kwa wanaume watajinyakulia kiasi cha shilingi milioni 4 kila mmoja,
shilingi milioni mbili kwa washindi wa pili na shilingi milioni 1 kwa washindi
wa tatu. Washindi wa kwanza kwenye mbio ndefu za nusu
marathon (km 21) wanawake kwa wanaume watajinyakulia kiasi cha shilingi milioni
2 kila mmoja, shilingi milioni 1 kwa washindi wa pili na shilingi 500,000 kwa
washindi wa tatu.
Addison aliongeza kuwa medali na
t-shirt zitatolewa kwa wanariadha 500 wa kwanza kumaliza mbio za kilomita 42,
wanariadha 2,200 wa kwanza kumaliza mbio za nusu marathon na wanariadha 80 wa
kwanza kumaliza mbio za walemavu. Washiriki 3,000 wa kwanza kumaliza
mbio za kujifurahisha za Vodacom 5km Fun Run watapewa t-shirts baada ya
kumaliza mbio na watapata fursa ya kujishindia zawadi mbalimbali za kuvutia
kupitia droo.
Mbio hizi zinaratibiwa na kwa
kushirikiana na Riadha Tanzania, Chama cha Riadha Mkoa wa Kilimanjaro na
Kilimanjaro Marathon Club huku zikidhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager,
Vodacom Tanzania, GAPCO, Simba Cement, KK Security, Keys Hotel, TPC Sugar,
TanzaniteOne, CMC Automobiles Ltd, Kibo Palace Hotel, RwandAir, FNB Tanzania,
UNFPA na Kilimanjaro Water.
0 COMMENTS:
Post a Comment