Na Saleh Ally
Mabingwa wa soka Tanzania, Yanga
wamelazimika kumwaga kitita cha dola 10,000 (zaidi ya Sh milioni 16) kuwapa Al
Ahly kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa Afrika,
Jumamosi.
Timu hizo zitapambana kwenye Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam na tayari mabingwa hao wa Afrika wametua nchini, tayari
kupambana na mabingwa hao wa Tanzania waliopania kuuangusha mbuyu huo.
Habari za uhakika kutoka ndani ya Yanga chini ya Mwenyekiti Yusuf Manji na naibu wake, Clement Sanga zinaeleza kwamba, uongozi wa Yanga umeukabidhi ule wa Al Ahly fedha hizo kwa
ajili ya matumizi yao watakapokuwa nchini kwa kuwa walikataa hoteli
waliyopangiwa.
“Yanga ilitumia kiasi hicho cha fedha
kuwalipia hoteli Komorozine ya Comoro ilipokuwa nchini, sasa Ahly wakaikataa
hoteli wakitaka wapangiwe Kempinsky, kitu ambacho kingekuwa ni gharama kubwa
sana na Yanga ikakataa.
“Kwa kuwa ilitenga hiyo dola elfu kumi,
basi ikawakabidhi Al Ahly na wenyewe ndiyo wameongezea na kwenda kupanga katika
hoteli wanayoitaka. Hivyo Yanga nayo inaweza kulipwa fedha au kupewa hoteli ya
kiwango hicho itakapokwenda Cairo,” kilieleza chanzo hicho cha uhakika.
Tayari watu wawili wametangulizwa nchini
kufanya maandalizi ya mechi hiyo dhidi ya Yanga na juzi na jana walikuwa kwenye
hoteli hiyo ya Kempinski kuweka mambo sawa pamoja na Uwanja wa Shule ya
Sekondari ya Kimataifa ya Tanganyika (IST) tawi la Upanga jijini Dar es Salaam
kuhakikisha wanafanya mazoezi kwenye uwanja wenye kiwango wanachoamini ni bora.
0 COMMENTS:
Post a Comment