Siku chache baada ya kufanikiwa kuiondoa Yanga kwenye Ligi ya Mabingwa
Afrika, Al Ahly imeonyesha kuwa na nia ya kurejea Tanzania tena na tena, baada
ya kutuma wawakilishi wake kuanza mchakato wa kumsajili chipukizi kutoka
Mwanza.
Taarifa ambazo zimefika mezani kwa Championi Ijumaa zimeeleza kuwa, Al
Ahly ambao ni mabingwa wa Misri na Afrika, wameonyesha nia ya kumwania Athanas
Mdamula ambaye anamilikiwa na kituo cha kukuzia soka cha Alliance School Sports
Academy (ASSA).
Mbali na Al Ahly, klabu nyingine ambayo imetajwa kumwania mchezaji
huyo ni Azam FC.
Chipukizi huyo ambaye ni mshambuliaji na mwenye uwezo wa kucheza
nafasi ya kiungo mshambuliaji, aliitwa katika kikosi cha Taifa Stars
kilichocheza dhidi ya Namibia na kutoka sare ya 1-1 na inaelezwa kuwa
alionyesha kiwango kizuri.
Akizungumzia suala hilo, Mkurugenzi wa ASSA, James Bwire, aliyekuwa
kwenye Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, alipomsindikiza mchezaji huyo
kuonana na Mkuu wa Wilaya hiyo, Baraka Konisaga, alisema klabu zote hizo
zimeonyesha nia ya kumsajili Mdamula.
“Nimesikia alipokuwa Namibia alionyesha uwezo wa juu, sasa wale Al
Ahly walikuwa na watu wao kwenye mechi ile, wakaomba mawasiliano yake, wakapewa
namba yangu kwa kuwa mimi ndiyo ninamlea Mdamula na wenzake wengi.
“Walinipigia simu wiki iliyopita, wakaomba kuonana na mimi lakini
wakati huo tayari walikuwa wamesharejea Misri, wakasema watakuja Tanzania na
tukutane Dar es Salaam, lakini mimi nikawaambia waje Mwanza, wakasema
watazungumza na uongozi wao kisha watanijulisha.
“Lakini Azam pia walinipigia simu, alinipigia yule nani yulee meneja
wao, nanii yulee ahhh! Jina limenitoka, ilikuwa hata kabla ya kwenda Namibia,”
alisema mkurugenzi huyo na kuongeza:
“Hata tulipoenda Kenya kwenye mashindano ya vijana, uongozi wa
Shirikisho la Soka Kenya (KFF) uliomba mchezaji huyo abadili uraia ili aichezee
timu yao ya taifa.”
Alisema Mdamula ana umri wa miaka 17 na kama kuna klabu itatimiza
masharti ya kumhitaji, hawatasita kumuuza, huku akitaja moja ya vigezo ni
kuhakikisha anasomeshwa kwa kuwa bado anasoma.
0 COMMENTS:
Post a Comment