March 4, 2014


KUNA maswali mengi kuhusiana na wachezaji wengi ambao huonekana wamekwisha ahapa nyumbani, lakini baadaye wanakwenda sehemu nyingine na kufanikiwa kufanya vizuri kabisa katika ligi mbalimbali za soka.


Pia kuna wachezaji huonekana wamekwisha, lakini wakiondoka kwenda kucheza nchini huonekana ni bora na baadaye wakarudi hapa nchini na kutoa msaada katika klabu kadhaa huku wakizinyanyasa timu zilizowaacha hapo awali.

Lakini kumekuwa na tabia moja ambayo inatokea mara nyingi sana, inawezekana katika timu nyingi za soka lakini zile za Ligi Kuu Bara na hasa wakongwe Yanga na Simba, zinaongoza kuwatoa wachezaji wao mchezoni kwa madai kuwa ‘wamekwisha’.

Tofauti ya mashabiki wa Yanga na Simba na wale wa timu nyingine kubwa huwa ni uvumilivu na pia subira. Kwamba wao wakisikia wanaamini, hawawezi kulifuatilia jambo au kukumbuka kabla, basi suala hilo linazagaa na kila mmoja analishika kulisambaza.

Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ alikuwa katika kipindi kigumu, takribani miwili iliyopita hakuwa katika wakati mzuri, taarifa za kwisha kwake zilizagaa. Siku chache alizowekwa benchi zilisababisha taarifa hizo kuchukua nafasi kubwa zaidi.

Kitu kibaya zaidi ni baadhi ya watu wenye nafasi kama viongozi, ingawa ni wale ambao si wa kuchaguliwa, walikuwa wanazungumza maneno kama hayo kuwa Cannavaro ameisha. Kwa baadhi ya mashabiki wakisikia fulani anazungumza, ni lahisi sana kuamini.
Baada ya hapo na wenyewe wanaamka na kuanza kutanguliza dharau na wakati mwingine hata kumzomea mchezaji huyo wakiamini ameisha na hana msaada na timu yao. Hakuna hata mmoja wao anaweza angalau kidogo akafikiria kitaalamu kuwa Cannavaro ni binadamu.

Binadamu ana mambo mengi, huenda alikuwa majeruhi na sasa ndiyo amerudi hivyo anahitaji muda kidogo, au ana matatizo ya kifamilia ambayo yanampa wakati mgumu na anahitaji kupumzika kidogo na kuyamaliza halafu aendelee na kazi yake.

Mashabiki wa zilizoendelea kisoka, wako tena wengi wanaoweza kuelewa hivyo na kumpa mchezaji nafasi. Liverpool wanaweza kuwa mfano mzuri kupita beki Jamie Carragher ambaye alikuwa anaongoza kwa kujifunza. Lakini walimpa sifa yake siku zote kwa kuwa alikuwa bora katika kuokoa na juhudi au hali ya kujituma ilikuwa juu.
Cannavaro hali kadhalika, anajulikana alivyo makini uwanjani, hataki mzaha. Ikitokea amekosea ni kama bindamu na mashabiki wanapaswa kumsamehe angalau mara moja. Ingawa si wote, wako wachache ambao wamekuwa adui wa timu zao wenyewe bila ya kujua.
Sasa Cannavaro ni shujaa wa Yanga, pamoja na kuokoa, ndiye alifunga bao pekee katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Yanga kuwalaza vigogo Al Ahly kwa bao 1-0. Swali, vipi waliosema Cannavaro ameisha, tena kwa kukurupuka, au walimzomea kwa kuamini maneno ya fulani, wanajisikiaje?

Hivi karibuni, Cannavaro alifunga bao katika moja ya mechi za Ligi Kuu Bara, Yanga ilikuwa inawavaa Ruvu Shooting. Alipoinuka wakati wa kwenda kushangilia, aliweka kidole mdomoni, ikiwa ni ishara ya kuwanyamazisha wale wenye midogo bila ya vipimo. Tena alielekea kwa mashabikiw a Yanga, ana haki ya kufanya hivyo.
Kama kitu hauna uhakika nacho, kaa kimya na fanya uchunguzi, ukishindwa, basi bora uzidi kukaa kimya. Wachezaji wengi wa Simba, Yanga wameondoka mchezoni wakiwa bado na uwezo. Lakini maneno ya viongozi wanaofanya kazi zao kishabiki pia mashabiki wenyewe yamewaondoa njiani.

Imekuwa namna hii, mashabiki kupitia baadhi ya viongozi wanaoamini wanajua sana mpira na kumbe hawajui lolote wamekuwa wepesi kusambaza mchezaji fulani amekwisha na baada ya muda wanasababisha mashabiki husika wa timu hiyo kuanza kumzomea uwanjani.

Wanaomzomea hufanya hivyo wakati akiichezea timu yao, labda Yanga au Simba, maana yake wanamchanganya na mwisho wao ndiyo wanaosema amekwisha. Wakati wakifanya hivyo, hakuna hata mmoja wao anayekuwa akikumbuka kwamba mchezaji huyo amekuwa msaada kwa kipindi kirefu.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic