Na Saleh Ally
KUTANGAZWA kwa Lionel Messi kuwa
mwanasoka anayeingiza kipato zaidi kuliko wengine wote duniani, kunazidi
kuipaisha Ligi Kuu ya Hispania ‘La Liga’ kuwa ndiyo yenye fedha nyingi zaidi.
La Liga ndiyo ligi inayotumia fedha
nyingi zaidi kuliko nyingine yoyote kutokana na mambo matatu. Kuwa na wachezaji
walionunuliwa kwa fedha nyingi zaidi, kulipwa juu zaidi, lakini klabu zake
mbili ni tajiri zaidi.
Inawezekana Ligi Kuu England
‘Premiership’ ikawa maarufu kutokana na timu nyingi zenye umaarufu tofauti na
Hispania ambayo ni Real Madrid na Barcelona, angalau kidogo kwa sasa Atletico
Madrid.
Lakini La Liga inabaki palepale,
malipo makubwa kwa wachezaji wake au umaarufu wao unaifanya ligi hiyo kukosa
mpinzani wa karibu kwa umaarufu kifedha.
Messi ametangazwa kuwa mchezaji
anayelipwa zaidi kufuatia kitita cha euro milioni 41 (Sh bilioni 93)
anachoingiza kwa msimu mmoja kutokana na malipo ya mshahara, marupurupu pamoja
na matangazo.
Vyombo vya habari vya Hispania,
vimetangaza, Cristiano Ronaldo anafuatia nafasi ya pili baada ya Messi ambaye
anapata zaidi kutokana na mkataba wake mpya na Barcelona.
Ronaldo anashika nafasi hiyo akiwa anaingiza
euro milioni 39.5 (Sh bilioni 89.3), halafu baada ya hapo ni Neymar wa Barcelona
anayepata euro milioni 29 (Sh bilioni 66) kwa kila msimu.
Hapa utaona, wachezaji watatu kutoka
La Liga ndiyo wanashika nafasi tatu za juu kwa kipato. Hii ni sehemu ya
kuonyesha kuwa ligi hiyo ni ghali zaidi na bado timu zake zinaendelea kuwa juu
zaidi kifedha.
Baada ya hao watatu, England inapata
nafasi ya nne kupitia Wayne Rooney wa Manchester United ambaye anaingiza euro
milioni 24 kwa msimu mzima, halafu sasa ngoma inahamia Ufaransa ambako Zlatan
Ibrahimovich wa PSG anaingiza pauni milioni 23.5.
Falcao wa AS Monaco anaingiza euro
milioni 21.1, anashika nafasi ya sita. Anafuatiwa na Kun Aguero wa Man City
anayepata pauni milioni 19.7.
Beki pekee anayeingiza fedha nyingi
zaidi duniani ni Thiago Silva wa PSG ya Ufaransa, kwa msimu anapata pauni
milioni 17, Eden Hazard wa Chelsea ni kinda mwingine milionea kwa maana ya
kipato cha msimu, anapata euro milioni 16.8 halafu Franck Ribery ndiye mchezaji
pekee kutoka Ujerumani kwenye Bundesliga aliyeingia kwenye 10 bora, anaingiza
euro milioni 16.5.
Hii inaweza kuwa sehemu ya kusoma
walakini kwamba Premiership ni ligi ya soka maarufu zaidi duniani. Sawa,
inawezekana kwa kutazamwa tu, lakini vipi watangazaji ambao pia wanahitaji watu
wanakwenda kutangaza zaidi Hispania?
Unapokwenda kwenye klabu tajiri, tatu
bora kuna timu mbili za La Liga ambazo ni Real Madrid na Barcelona na
Manchester United pekee kutoka England imekuwa ikijitutumua.
Au ufinyu wa timu nyingi zinazofanya
vizuri ndiyo unaoibana La Liga, maana ina Barca na Madrid pekee. Wakati England
inaweza kujitanua na Big Four au zaidi.
Yote hayo yanaweza yakawa yanapita tu,
mijadala ikawa ni ya kila aina lakini ukweli ni hivi; fedha za soka ziko La
Liga ambao ndiyo wakiamua kulipa kwa ajili ya kununua au mshahara, basi
wanafanya kweli.
Mchezaji anayetaka kuwa tajiri kupitia
soka, tena tajiri wa kiwango cha juu, hakuna ubishi, lazima apitie La Liga.
Pamoja na kuwa na timu tajiri zaidi,
wachezaji wanaolipwa zaidi, lakini La Liga wanaendelea kushikilia rekodi ya
wachezaji walionunuliwa kwa fedha nyingi zaidi. Ilikuwa Ronaldo na sasa Gareth
Bale halafu Neymar.
Sifa zinaweza kugawanyika kwa kuwa si
rahisi kila kitu kupatikana sehemu moja, lakini kama fedha, karibia La Liga.
0 COMMENTS:
Post a Comment