April 2, 2014

POULSEN WAKATI AKIWA KAZINI NA TAIFA STARS
Hatimaye Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limefutiwa aibu kubwa na Serikali baada ya kulipiwa deni alilokuwa anadai kocha wa timu ya taifa, Taifa Stars, Kim Poulsen.


Hivi karibuni, (TFF) lilimfungashia virago aliyekuwa kocha mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen kutokana na kile kilichodaiwa ni kutoridhishwa na uwezo wake wa ufundishaji.

Rais wa TFF, Jamal Malinzi, alisema madai yote ya kocha huyo yatalipwa na wadau wa shirikisho hilo na mmojawapo akiwa ni yeye mwenyewe lakini kocha huyo aliendelea kukaa nchini kwa zaidi ya wiki kadhaa huku habari zikidai kuwa wadau wale wameepa kulipa fedha hizo.

 Hata hivyo, baada ya hali kuwa mbaya huku Poulsen ambaye kabla hajavunjiwa mkataba wake na TFF alikuwa akilipwa na Serikali, akiendelea kusota hapa nchini bila ya mafanikio, Serikali ilibidi iingilie kati ili kuifichia aibu TFF juu ya jambo hilo.

Habari za uhakika ambazo Championi Jumatano limezipata kutoka chanzo cha kuaminika ndani ya TFF, zimesema kuwa baada ya Serikali kuona hivyo huku kocha huyo ambaye alikuwa amebakiza mkataba wa mwaka mmoja wa kuifundisha Taifa Stars akiendelea kusota hapa nchini, ilibidi iingilie kati na kuamua kumlipa  ili aondoke kwenda kuendelea na shughuli zake.

“Baada ya Serikali kuchukua jukumu hilo la kumlipa Poulsen madai yake hayo ambayo alikuwa akiidai TFF, ndipo alipoamua kuondoka nchini na kurudi kwao nchini Denmark.

“Kutokana na hali hiyo, TFF sasa ndiyo itakayoilipa Serikali fedha hizo na haina ujanja juu ya suala hilo, ni lazima itazilipa watake wasitake kwani ni nyingi sana,”  kilisema chanzo hicho.

Chanzo hicho kilisema kuwa , Poulsen alikuwa akiidai TFF, karibia Sh milioni 200,  kama malipo ya mshahara wake ya miezi yote aliyokuwa amebakiza katika mkataba wake.


Mbali na fedha hizo pia chanzo hicho kilisema kuwa Poulsen alikuwa akidai fedha nyingine kutokana na kwenda kinyume na makubaliano ya mkataba wake.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic