Siku chache
baada ya mshambuliaji wa kimataifa wa Simba, Amiss Tambwe, kutangaza kuikacha
timu hiyo kutokana na ndoto zake za kutaka kushiriki michuano ya kimataifa
kufeli, sasa yupo mbioni kujiunga na Azam.
Tambwe
ambaye anaongoza kwa kuzifumania nyavu katika michuano ya ligi kuu msimu huu
akiwa na mabao 19, amesema
yupo tayari kutua klabuni hapo mara tu mipango yake itakapokamilika.
Tambwe amesema kuwa taratibu za kujiunga na Azam
zimepamba moto na tayari ameshafanya nao mazungumzo kupitia kwa wakala wake.
Alisema Azam wanataka kumsajili ili waweze
kuimarisha safu ya ushambuliaji ya kikosi chao kwa ajili ya michuano ya Ligi
Kuu Bara msimu ujao na ile ya Klabu Bingwa Afrika endapo itafanikiwa kumaliza
ya kwanza katika kivumbi cha ligi kuu msimu huu.
“Baada ya
kuzungumza na wakala
wangu aliwaambia kuwa mimi nipo tayari kujiunga nao ila wanapaswa kumalizana na
Simba kwanza kwa sababu bado nina mkataba nao, hivyo siwezi kufanya lolote bila
yao kuridhia.
“Lakini kwa
upande wangu sina tatizo lolote na endapo nitajiunga na Azam, kwangu litakuwa
ni jambo jema na nitafurahi,” alisema Tambwe ambaye alijiunga na Simba mwanzoni
mwa msimu huu akitokea Vital’O ya Burundi.
Hivi karibuni Tambwe aliliambia gazeti hili kuwa anataka kuondoka Simba kwa kuwa nia
yake ni kucheza michuano ya kimataifa.
Hata hivyo,
Katibu Mkuu wa Azam, Idrissa Nassor, alipoulizwa
juu ya suala hilo, alisema kuwa kwa sasa hawezi kulizungumzia lakini ikitokea
akampata Tambwe basi litakuwa ni jambo
jema kwao.
“Tambwe ni mchezaji mzuri na kila kiongozi wa
timu angependa kuwa na mchezaji kama yeye lakini kwa sasa siwezi kuzungumza
lolote kuhusiana naye kwani bado ni mali ya Simba lakini endapo itatokea
tukampata itakuwa ni jambo zuri na jema kwetu,” alisema Nassor.
Kweli anae wahonga kuivuruga Simba anajitahidi, sema ndio ilivyo kila mbuzi anakula kutokana na urefu wa kamba yake, ila kuivuruga Simba hamuwezi, mlishindwa mapinduzi iwe hili, kwisha habari yenu mbulula nyie
ReplyDelete