Na Saleh
Ally
PAMOJA na
mambo mengi lakini hakuna ubishi kuwa Azam FC ndiyo timu yenye uhakika wa
kumtwaa beki wa zamani wa Simba, Shomari Kapombe.
Kapombe
ambaye alikuwa akikipiga nchini Ufaransa katika kikosi cha AS Cannes
kinachoshiriki ligi Daraja la Nne nchini humo, tayari amerejea nchini na
amekuwa akifanya mazungumzo na Azam FC.
Kawaida,
Kapombe amekuwa mgumu kuzungumza lakini taarifa za kiuchunguzi za gazeti hili zimekuwa
zikieleza namna mazungumzo kati ya Kapombe na Azam yanavyoendelea na hivi
karibuni imebainika ameishavunja mkataba na AS Cannes.
Kinachomkwamisha
ni kuwepo mgogoro wa malipo ya fedha zake za mshahara kutoka kwa AS Cannes,
lakini bado kwa mujibu wa sheria za Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa),
Kapombe ana nafasi ya kusajili katika timu mpya.
Beki huyo
kiraka alianza kung’ara na Simba ndipo AS Cannes kupitia wakala wa kuuza
wachezaji anayetambuliwa na Fifa, Denis Kadito ambaye ni Mtanzania anayeishi
nchini Uholanzi, ikamnasa na kuanza naye kazi.
Hata hivyo,
Kapombe hakuwa katika wakati mzuri baada ya kujikutana safari yake ina
misukosuko kibao pale alipoumia na kufanyiwa upasuaji wa kidole akiwa Ufaransa,
hali iliyomlazimu kukaa nje kwa zaidi ya mwezi mmoja.
Aliporejea,
alionyesha kiwango kizuri na kufanikiwa kupata namba huku benchi la ufundi la
AS Cannes likimuamini na kumpa namba mbili au beki wa kulia.
Lakini
taratibu migogoro ilianza baada ya
kurejea nyumbani kuichezea timu ya taifa, Taifa Stars dhidi ya Zimbabwe.
Akachelewa kurudi na baadaye akatangaza kwamba anadai mshahara wake, mgogoro
haukupoa mapema hadi ilipoelezwa Wafaransa hao wako tayari kumlipa.
Lakini
baadaye Kapombe akashikilia msimamo wa kutaka kubaki nchini, kazi ya kuvunja
mkataba na AS Cannes ikaanza na baadaye taarifa za Yanga na Azam FC kuanza
kumuwania zikajulikana.
Baadaye
ikaonekana Azam FC ndiyo wamekuwa ‘siriaz’ na suala la kumnasa Kapombe. Baadaye
Simba wakaingilia na kudai bado Kapombe ni mchezaji wao, lakini bado
hawakuonyesha kweli wako ‘siriaz’ kama ilivyo kwa Azam.
Kapombe
amekuwa akijificha na kutotaka kulizungumzia suala lake, lakini Championi
Jumatano lilifanikiwa kumpata na kufanya naye mazungumzo kwa ufupi.
Kapombe
anasisitiza kweli ameamua kurejea nchini na anajua baada ya muda itajulikana
anachezea timu gani lakini akitaka watu wawe na subira kwa kuwa mazungumzo
yanaendelea ingawa dalili zote zinaonyesha kuwa itakuwa ni Azam FC. Msome
anavyofafanua maswali.
Simba:
Ningependa
sana kufanya mazoezi na Simba kwa kuwa ndiyo timu niliyotoka na sina matatizo
nao, lakini kuna vifaa ambavyo ninavihitaji nisingeweza kuvipata lakini kwa
Azam inakuwa rahisi kwa kuwa wana vifaa vya kutosha.
Pamoja na
hivyo, kuna jambo la kocha, angalia mwendo wa Simba na aina ya kocha wao
(Zdravko Logarusic), ni mkali sana wakati mwingine anawaweka nje wachezaji
ambao ni wake.
Kwa hali ya
kawaida tu kama binadamu nikaingia hofu, nikajiuliza kama kweli wachezaji wakikosea
kidogo anawaadhibu au kuwaondoa mazoezini. Kwa mimi ambaye sijasajiliwa, lengo
langu ni mazoezi, nitaweza kufanya mazoezi kwa uhakika na utulivu?
Azam:
Suala la
Azam wananitaka au la, nisingependa liwe ndiyo gumzo. Lakini kweli nimeomba
kufanya mazoezi kwao kwa kuwa ninajua nitapata kila kitu.
Lengo langu
ni kuwa fiti na ikifikia nimekubaliana na timu fulani kuichezea na kuingia nayo
mkataba, basi niwe katika kiwango kizuri kuliko kukaa tu ninasubiri.
Kingine ni
suala la gharama, mfano pale kwenye Uwanja wao Azam, wana gym. Lakini kama
ningefanya mazoezi na Simba, ningelazimika kuwa na fungu la kulipia gym tena
sehemu nyingine.
Kwa sasa
mimi sina sehemu inayoniingizia, hivyo siwezi nikawa ninatoa tu fedha bila ya
kuingiza. Kwa kutumia vifaa vya Azam kwa kuwa vimekamilika, nitapunguza gharama
na kufanya mazoezi ya uhakika.
Kurudi
Ulaya:
Nimeamua
kubaki hapa nyumbani na kweli kuna timu ambazo ninafanya nazo mazungumzo,
hakuna upande ambao kila kitu kimekamilika, lakini baada ya muda nitaeleza kila
kitu.
Nataka
nikuhakikishie, sijawahi kuzungumza na mwandishi na kumueleza mambo mengi,
angalau leo. Lakini mara baada ya kukamilisha suala usajili na nikiwa nimejua
ninakwenda wapi, basi nitakuwa tayari kuzungumza.
Safari
yangu ya Ufaransa ina mambo mengi sana, nitazungumza kuanzia nilivyoondoka
hapa, nilivyofika na kufanya majaribio na mambo yote yatakavyokwenda. Hivyo
vuteni subira kidogo.
Gharama:
Kweli kuna
gharama za matibabu kama Cannes ambavyo wamekuwa wakisema, lakini mimi
nilikataa kufanyiwa oparesheni. Unajua lilikuwa ni lengelenge tu, haikuwa ni
mara ya kwanza kunitokea, hivyo nikawaambia sitapasuliwa.
Unajua hapa
nyumbani hicho ni kitu cha kawaida tu, halafu unachofanya unatoa kile kingozi
cha juu unaendelea na mambo yako. Lakini wao wakaona ni tatizo na lazima iwe
vile, nikawakubalia.
Lakini
subiri kwanza nimalize mambo yangu kama nilivyosema, halafu nitatoa ufafanuzi
wa kutosha kuhusiana na suala hilo na mengine mengi.
0 COMMENTS:
Post a Comment