April 2, 2014


Na Saleh Ally
KADIRI siku zinavyosonga mbele, mambo kwenye Ligi Kuu England yanazidi kuwa kama filamu ambayo ‘steringi’ wake hajulikani kutokana na ugumu na kutokuwa na uhakika itakavyokwisha.

Awali ilionekana Arsenal ndiyo yenye nafasi kubwa ya kubeba ubingwa wa ligi hiyo maarufu kama Premiership. Lakini baadaye mambo yakabadilika, Chelsea na Man City zikawa juu na nafasi kubwa.

Lakini sasa, Liverpool imerejea kileleni, pia inaonekana ina nafasi ya kufanya vizuri na kubeba kombe hilo kama hesabu zake zitakaa vizuri katika mechi sita za mwisho zitakazochezwa ndani ya siku 34.
Siku hizo 34 kama kweli Liverpool itajipanga vizuri, basi inaweza kuwashangaza wengi na kubeba ubingwa wa Premiership huku ikimaliza ukame wa kombe la ligi hiyo kwa zaidi ya miaka 20 sasa.

Katika mechi sita zilizobaki, tatu zitakuwa nyumbani na zilizobaki ugenini. Hivyo Liverpool ina nafasi kubwa ya kufanya vizuri na kufanikiwa kuwa mabingwa wapya wa England.
Unaweza kuipuuzia Liverpool, lakini ina mambo mengi ambayo yanaonyesha ina nafasi ya kuchukua ubingwa kwa maana ya mabao ya kufunga, mechi zilizopita na mengine.
Mechi:
Kiwango cha ushindi wa mechi nyingi zaidi kinashikiliwa na Liverpool ambayo tayari ipo kileleni.
Baada ya mechi 32, Liverpool imeshinda 22 na ndiyo timu iliyoshinda nyingi zaidi kuliko nyingine yoyote katika msimamo wa Premiership.
Chelsea na Man City wanafuatia kwa kushinda mechi 21 kila mmoja na timu zote tatu zinalingana katika mechi zilizopoteza. Kila moja imepoteza tano.

Ushindi:
Katika mechi nane zilizopita, Liverpool ndiyo timu pekee yenye rekodi ya juu ya ushindi. Imeshinda mechi zake zote nane zilizopita na hakuna timu nyingine iliyofanya hivyo.
Chelsea inayowafuatia, katika mechi nane imeshinda mechi tano, sare moja na imepoteza mbili na zilizosaidia Liverpool ichukue uongozi.
Pamoja na kwamba Man City ina mechi mbili mkononi, lakini katika mechi zake nane zilizopita, imeshinda tano, imepoteza moja na sare mbili.

Mabao:
Bado Liverpool ina rekodi nyingine nzuri ya kufunga mabao mengi zaidi kuliko timu yoyote katika msimamo wa sasa wa Premiership.
Imefunga mabao 88 huku timu inayoifuatia angalau kwa karibu ni Man City ambayo ina 80. Hii inaonyesha kasi ya ufungaji ya SAS, yaani Sturridge na Suarez iko juu.
Chelsea ndiyo wanashika nafasi ya tatu kwa mabao ya kufunga, mabao 62, hii inaonyesha kiasi gani Liverpool ni hatari kwa upachikaji mabao.

Pointi 3:
Sehemu muhimu kwa Liverpool ni pointi tatu kutoka kwa Man City ambao watacheza nao Aprili 13, kama wakizibeba, maana yake watakuwa wamewapunguza kasi hali kadhalika Chelsea ambao watacheza nao Aprili 27.

Mechi zote mbili Liverpool itakuwa nyumbani Anfield, kiasi fulani wana nafasi zaidi. Lakini kwa kuangalia mechi zilizopita, bado wana nafasi ya kushinda mechi yoyote kati ya hizo.
Hivyo hesabu za uhakika za zaidi kwa Liverpool, zinatakiwa zifanyike kuhakikisha inapata pointi tatu mara mbili za vigogo hao ili kuua ndege wawili kwa jiwe moja.


MECHI ZILIZOBAKI
West Ham Vs Liverpool
Liverpool Vs Man City
Norwich Vs Liverpool
Liverpool Vs Chelsea
Palace Vs Liverpool
Liverpool Vs Newcastle
Fin.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic