Katibu Mkuu wa Shirikisho la
Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Jerome Valcke atawasili nchini Mei 1 mwaka
huu ambapo atafungua semina ya mawasiliano itakayoshirikisha viongozi wa vyama
wanachama wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati
(CECAFA).
Akizungumza Dar es Salaam leo (Aprili
14 mwaka huu), Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal
Malinzi amesema Valcke ambaye hii ni mara yake ya kwanza kuja Tanzania
atafuatana na maofisa wengine wa saba wa FIFA.
Amesema semina hiyo iliyoandaliwa na
FIFA itafanyika kwa siku mbili (Mei 1 na 2 mwaka huu) ambapo vilevile Valcke
atapata fursa ya kuzungumza na waandishi wa habari wa ndani na wa kimataifa.
Rais Malinzi amesema washiriki wa
semina hiyo ni marais, makatibu wakuu na wakuu wa mawasiliano wa wanachama 12
wa CECAFA ambao ni Burundi, Djibouti, Eritrea, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Somali,
Sudan, Sudan Kusini, Tanzania na Uganda.
Naye Mwenyekiti wa CECAFA, Leodegar
Tenga ambaye alifuatana na Katibu Mkuu wake Nicholas Musonye amemshukuru Rais
wa TFF kwa kukubali kuwa mwenyeji wa semina hiyo kwani itasaidia katika
maendeleo ya mpira wa miguu katika ukanda huu.
0 COMMENTS:
Post a Comment