Na Saleh
Ally
INAWEZEKANA
kabisa kwamba wakati mwafaka kwa Arsenal umewadia, itafuta ukame wa makombe
bila ya kujali ni la Premiership, FA au Kombe la Ligi.
Mara ya
mwisho Arsenal kutwaa kombe kati ya hayo matatu yanayotambulika England ni
mwaka 2005 na lilikuwa ni Kombe la FA.
Baada ya
hapo, Arsenal chini ya Arsene Wenger wamekuwa wakiyashuhudia makombe hayo
kwenye ‘kideo’, taratibu miaka imesonga mbele hatimaye imefika kipindi sasa
inaonekana kama makombe kwao ni hadithi na ndiyo kitu cha ‘kuwasimangia’.
Lakini
kutiga fainali juzi kwa changamoto ya mikwaju ya penalti baada ya sare ya bao
1-1 huku Fabiasnki akiokoa penalti mbili na kuwa shujaa, kunaonyesha kuwa
Arsenal sasa wanaweza kubadili upepo huo wa kusimangwa.
Kwamba ni
timu inayogombea nafasi nne za juu ili kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya na si vinginevyo,
kwani hata ubingwa wa Premiership mara ya mwisho ilikuwa ni msimu wa 2003-04.
Baada ya
hapo hakuna makombe, mfumo wa kikosi chake ni kucheza soka la kuvutia,
inaongoza ligi mwanzoni na inapofikia hatua za mwisho, taratibu inaanza kupiga
‘rivasi’ hadi kushika nafasi angalau ya tatu au hata ya nne kabisa!
Safari hii
katika Premiership, hali hiyo imeanza kujitokeza, kweli Arsenal imeporomoka
hadi kufikia katika nafasi ya tano, wakati ilikuwa inaongoza kwa tofauti ya
pointi zaidi ya 10.
Inawezekana
wakati wa kufuta makosa, wakati wa kubadilika au kufuta ‘nuksi’ umewadia. Maana
Arsenal imefanikiwa kuingia fainali ya Kombe la FA baada ya miaka nane, mara ya
mwisho ilikuwa mwaka 2005 ilipoingia fainali dhidi ya Man United na kushinda
kwa mikwaju 5-4 ya penalti baada ya dakika 90 zenye majibu ya 0-0.
Sasa
wamerudi tena, fainali ni dhidi ya Hull City inayokipiga Ligi Kuu England,
lakini Arsenal wanachotaka ni kombe.
Kombe kwa
Arsenal ni sawa na dawa, ni sawa na gia mpya ya kuanza maisha mapya kwamba ni
timu bora ambayo inaweza kuchukua makombe na si pasi nyingi na soka la kuvutia
lakini kila msimu wanaibuka patupu.
Ukiangalia
uwezo wa kikosi uko juu, utaona mechi ya nusu fainali dhidi ya Wigan ilivyokuwa
ngumu hiyo juzi, lakini Arsenal ikaweza kuhimili na kusawazisha na baadaye kuvuka
kwa mikwaju ya penalti.
Bado Arsenal si ya kuidharau kama utaihusisha
na kombe hilo kongwe kuliko mengine yote ya England. Imelitwaa mara 10 na
inazidiwa na Man United pekee ambayo imelibeba mara 11, hivyo hii inaonyesha
ina nafasi kwa maana ya rekodi.
Lakini
rekodi pekee hazilipi kila kitu, kwani Arsenal imeingia fainali mara 18 na
kufanikiwa kulibeba kombe hilo mara 10. Maana yake imepoteza fainali nane
ikiwemo ya mwaka 2001 dhidi ya Liverpool ambayo vijana wa Wenger walilala kwa
mabao 2-1.
Wenger,
mwenyewe ana rekodi ya kulibeba kombe hilo mara nne, si haba, kwani alipotua
mwaka 1996 akitokea Japan, miaka miwili baadaye akalibeba na baada ya hapo
akaongeza mara tatu, 2002, 2003 na 2005.
Maana yake
katika miaka ya 2000, tayari Arsenal imebeba kombe hilo mara tatu pamoja na
kwamba sasa imelikosa mara nane, huu unaweza kuwa msimu mzuri kwake kulibeba na
kulitumia kama dawa ya kubadili mwelekeo na kuachana na ule wa kutobeba makombe.
Presha
kubwa ya Arsenal ni makombe, hata wale mashabiki wanaolaumu kuhusiana na Wenger
ni kwa kuwa kikosi chao hakibebi makombe ukilinganisha na wapinzani wao
Manchester United na hata Liverpool ambayo pamoja na kukosa ubingwa wa Ligi Kuu
England kwa miaka zaidi ya 20, lakini angalau wanajikongoja na kufikia kubeba
hadi ubingwa wa Ulaya.
Lakini
presha inazidi kupanda zaidi kwa Arsenal ambao wanaamini ‘vijana’. Wakati Man
City na Chelsea nazo zikiendelea kufurukuta, Arsenal inaendelea kusuasua.
Fainali ya
Kombe la FA itakayopigwa Wembley Mei 17 ndiyo itatoa jibu kwamba Arsenal
imebadili mwelekeo au itaendelea kuchepuka njia kuu ya makombe bila ya kuchoka!
TIMU ZILIZOCHUKUA MARA NYINGI ZAIDI:
TIMU
MAKOMBE FAINALI
Man United 11 18
Arsenal 10 17
Tottenham 8 14
Aston Villa 7 13
Chelsea 7 13
Liverpool 7 11
ARSENAL IMETWAA FA MARA 10
FAINALI ZA
MIAKA YA 2000
2000 Chelsea Vs Aston Villa 1-0
2001 Liverpool Vs
Arsenal 2-1
2002 Arsenal Vs Chelsea 2-0
2003 Arsenal Vs Southampton 1-0
2004 Man United Vs Millwall 3-0
2005 Arsenal Vs Man United 0-0
(Dk 120)
Arsenal shinda penalti 5-4
2006 Liverpool Vs West Ham United (Dk 120)
Liverpool shinda penalti 3-1
2007 Chelsea Vs Man United 1-0
2008 Portsmouth Vs Cardiff City 1-0
2009 Chelsea
Vs Everton 2-1
2010 Chelsea Vs
Portsmouth 1-0
2011
Man City Vs
Stoke City 1-0
2012
Wigan Vs
Man City 1-0
0 COMMENTS:
Post a Comment