TAMBWE KAZINI |
Kocha Mkuu
wa Simba, Zdravko Logarusic, amesema litakuwa ni pigo kubwa kuondoka kwa
mshambuliaji wake, Amissi Tambwe mwishoni mwa msimu huu.
Loga
amesema itakuwa ni sawa na kuwa na adui kwenye nyumba yako mwenyewe kwa kuwa
Tambwe kwa sasa ndiyo staa kwenye kikosi cha Simba na timu hiyo haitakiwi kuuza
mchezaji bora bali kununua wachezaji bora.
Imeelezwa
kuwa timu ya Azam FC inamnyemelea mchezaji huyo kutokana na kuona anafaa
kuisaidia katika michuano ya kimataifa msimu ujao, lakini na Tambwe naye
amekiri kuwa anawasubiri mabingwa hao wapya.
Akizungumza
na Championi Jumatano, Loga alifunguka kuwa kikosi hicho kinahitaji marekebisho
makubwa msimu ujao na iwapo Tambwe ataondoka hali itakuwa tete kwa kuwa itakuwa
siyo nia yao sahihi.
“Tambwe ni
mchezaji mzuri na ameisaidia timu kwa kiasi kikubwa iwapo ataondoka hili
litakuwa pigo kubwa kwetu, huyu ndiyo staa kwetu na hilo halina ubishi.
“Siyo
taarifa rasmi kuwa anaweza kuondoka lakini kama akiondoka hakika atakuwa adui
kwetu kwa kuwa atakuwa anatufunga na kutuzuia kwenda mbele tunapotaka.
“Simba
inahitaji marekebisho makubwa msimu ujao ili kuweza kupata wachezaji wenye
viwango watakaoleta ushindani kwenye ligi na hatimaye kutwaa ubingwa lakini
siyo kuwauza wale bora,” alisema Loga.
Tambwe
amefanya kazi kubwa msimu huu akiwa ndiye kinara kwa ufungaji baada ya kufunga
mabao 19 hadi sasa ikiwa imebaki mechi moja.
Akizungumza
na Championi hivi karibuni Tambwe alisema kuwa bado nia yake ya kuondoka kwenye
kikosi cha Simba ipo palepale na anachosubiri ni timu yake hiyo imalizane na
Azam ambao wanamtaka.
“Mimi nipo
tayari kujiunga na Azam, lakini ninachosubiri ni wenyewe na Simba kukaa mezani
na kumalizana kwa kuwa mimi ni mchezaji wa Simba kwa sasa,” alisema Tambwe.
0 COMMENTS:
Post a Comment