Na Mwandishi Wetu
MAFANIKIO ndiyo majibu ya kufanya mambo
kwa juhudi na maarifa na mwanasoka yeyote anayetaka kufikia mafanikio, hawezi
kuridhika hadi wacheze kwenye vikosi vya timu zao za taifa.
Timu ya taifa ni sehemu ya kipimo cha
mafanikio kwa mwanasoka au mwanamichezo yoyote, kwamba umefikia kiwango cha juu
hadi kuwa mwakilishi wa taifa lako.
Bukaba Paul ni Mtanzania anayecheza soka
la kulipwa nchini DR Congo na amepita njia tofauti kufikia hapo alipo zaidi akiongozwa
na nia ya kutaka kupata mafanikio.
Mwanasoka huyo anayependwa kutumia jina
lake la kwanza la Bukaba sasa anakipiga katika timu ya OC Muungano inayoshiriki
Ligi Kuu nchini Dr Congo.
Bukaba ni kati ya wachezaji wachache
nchini ambao wamefanikiwa kutoka nje na kucheza soka la kimataifa bila ya
kuzichezea timu maarufu kama Yanga, Simba au Azam FC. Safari yake ilikuwaje
hadi kufikia alipo sasa?
“Haikuwa safari lahisi kwa kuwa ilikuwa
ni lazima kupita katika sehemu ambazo sikuwa na msaada zaidi ya mimi mwenyewe
kupambana,” anasema Bukaba kutoka DR Congo.
Hadi DRC:
Nilipambana sana, nilifanikiwa kufuzu
majaribio ya kuichezea Athletico Olympic ya Burundi, nilipambana na kufanikiwa
kupata namba na msimu huo tukamaliza ligi tukiwa wa pili nyuma ya Vital’O.
Baada ya msimu mmoja tayari nilianza
kuonekana na timu ya OC Muungano ilifanya mazungumzo na timu yangu ya Burundi
na baada ya muda mambo yakaenda vizuri nikaja hapa Congo. Hadi sasa naendelea
vizuri kabisa.
Kiwango:
Kama ni kiwango cha fedha hapa Congo
kipo juu zaidi ya Burundi na hata nyumbani Tanzania, hivyo ninapambana zaidi
ili nijiunge na timu kubwa zaidi za hapa au nchini nyingine.
Nyumbani:
Nilianzia nyumbani lakini kimyakimya
sana, nilianza kucheza soka nikiwa na miaka nane. Nilisoma kule kwetu Ukerewe,
nikiwa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Nakoza, nilichaguliwa katika
timu ya Taifa Cup ya Mwanza. Baada ya mashindano, Toto African waliniona
wakanisajili, wakati huo tayari nilikuwa ninacheza Nansio United ya kwetu
Ukerewe hiyo ilikuwa mwaka 2011.
Mwaka uliofuata nilipata nafasi ya
kucheza Kombe la Uhai chini ya miaka 20 nikiwa na mkoa wa Mwanza. Baada ya hapo
nilirejea na kuitumikia Toto kabla ya kwenda Burundi kufanya majaribio ambako
nilifuzu.
Anachotaka:
Kwa sasa natamani kuichezea timu yangu
ya taifa, Taifa Stars. Nina uwezo huo sema inakuwa vigumu kuniona, lakini
ningependa wasogee na kuniona ninapokuwa kazini.
Simba&Yanga:
Najua ni timu kubwa, niko tayari kama
watanihitaji. Kikubwa ni kufanya utaratibu na mimi nitaangalia kama maslahi wanayotangaza
yananifaa basi itakuwa vizuri.
Zaidi:
Pamoja na mambo yote, kweli natamani
sana kucheza soka Ulaya, hii ni ndoto yangu. Najua si kitu lahisi lakini
nitapambana hadi kuhakikisha nafika.
0 COMMENTS:
Post a Comment