LIGI Kuu Bara inaelekea ukingoni na
asilimia kubwa inaonyesha Azam FC huenda kwa mara ya kwanza itakuwa ndiyo
bingwa mpya wa Tanzania Bara.
Azam FC ambayo imeanzishwa katika
kipindi kifupi kisichofikia miaka kumi, sasa imekuwa tishio na kero kubwa kwa
timu kongwe za Yanga na Simba ambazo zimeanzishwa zaidi ya miaka 75 na
zimeshindwa kukua kwa maana ya maendeleo.
Simba na Yanga ndiyo kongwe, zina
mchango wao mkubwa katika soka nchini, lakini zina sehemu ambazo zimechangia
kwa kiasi kikubwa kudumaa kwa mchezo huo kama zile migogoro, kujenga makundi ya
watu wenye nguvu lakini wasiokuwa na changamoto za mafanikio kwenye soka.
Yanga na Simba, hadi sasa ni mfano mbaya
kwa kuwa zimeshindwa kumiliki hata uwanja wa kuingiza watu 20 ambao utakuwa na
sehemu nzuri ya kuchezea ambayo ni afya kwa wachezaji wao na mfumo wa kitaalamu
ili kwenda na wakati.
Leo utawaona Yanga wanalazimisha timu
yao kwenda kufanya mazoezi kwenye uwanja mbovu kabisa huku watani wao Simba
wakifanya porojo ya kupeleka watu kwenda kufyeka uwanja wao wanaoumiliki nje ya
jiji la Dar es Salaam ambako hakuna lolote la maana!
Sasa ligi inakwenda ukingoni huku
mabadiliko yakionyesha wakati wa mabadiliko ni sasa na kama kuna watu wabunifu
au wenye malengo ya kufanya mambo bora katika soka, si lazima wawe Yanga au
Simba pekee.
Wanaweza kwenda Mgambo FC, angalia
inakaribia kuteremka daraja lakini imeweza kushinda na kuzifunga Yanga na Simba
katika mechi zake mbili kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.
Ukilinganisha Mgambo dhidi ya Yanga na
Simba, karibu kila kitu timu hizo kongwe zitakuwa juu. Mfano, mishahara
mikubwa, kuwa na wachezaji wa kigeni, huduma kwa makocha na wachezaji lakini
Mgambo FC imeshinda.
Kikubwa ambacho kiliwabeba Mgambo
itakuwa ni nidhamu ya mazoezi, mfumo wa uongozi na nidhamu ya uwanjani kufuata
maelekezo kutoka kwa walimu wao, kitu ambacho kina matatizo katika timu nyingi
kubwa na hasa Yanga na Simba.
Inawezekana Yanga na Simba wakawa na
lawama nyingi kipindi hiki kwamba walihujumiwa katika mechi hizo au kulikuwa na
tatizo. Lakini mfumo na mwendo wa maisha ya klabu hizo na timu zake kuna tatizo
kubwa sana na lazima wakubali ili kujifunza na baadaye kubadilika.
Azam FC nao wanataka kuuchukua ubingwa,
pia kutakuwa na walakini kama Yanga au Simba watatanguliza lawama katika kitu
fulani kuhusiana na hilo. Badala yake waangalie na kukubali walipokosea na
kujifunza.
Dunia inabadilika kwa kasi sana, kuna
mengi ya kujifunza kila kukicha kwa kuwa watu wanajifunza na wanaelimika. Wako
tayari kufanya mambo mapya, hivyo lazima Yanga na Simba wajiangalie upya, la
sivyo wataishia kwenye lawama na mwisho utakuwa ni mwanzo wa kuanguka kwao.
Simba iko mbioni kugombea nafasi ya
tano, dalili zinaonyesha wakizubaa hata nafasi ya nne itakuwa kazi kubwa kwao.
Kuna la kujiuliza hapa na utaona chanzo kikubwa ni kutokuwa na uongozi imara,
uongozi uliokuwa ukilumbana kila kukicha na haufanyi mambo kwa manufaa ya timu.
Kwa wale wanaofanya mambo yao kishabiki
wanaweza kuwa wagumu sana kuamini au kukubali, lakini mwendo wa klabu zao si
mzuri kwa kuwa zinakwenda kwa mfumo wa kizamani, hazitaki kujifunza na
zinaamini sana historia kuliko hali halisi.
Kubadilika ni muhimu na moja ya mambo
yanayoweza kuonyesha kuwa watu wamekubali kuwa na mafanikio ni viwanja na vifaa
bora vya mazoezi, mfumo mzuri wa kudhibiti fedha ili kila inayopatikana itumike
kwa manufaa ya klabu.
Lakini pia kuwaachia makocha kama
wataalamu au wataalamu wengine kwenye klabu wafanye kazi zao si kwa matakwa ya
viongozi, badala yake kwa kufuata utalaamu. Azam FC inabadilisha mambo kidogo
tu na imeweza kufanikiwa na ukiangalia utaona ilipopitia ni kwenye mashimo
ambayo Yanga na Simba walishindwa kuyafukia.
0 COMMENTS:
Post a Comment