Sakata la mshambuliaji wa Yanga, Emmanuel Okwi kudaiwa kususia
mazoezi, sasa limeendelea mbele zaidi ya ilivyoelezwa awali.
Habari mpya ni kuwa Okwi, raia wa Uganda, amegoma kabisa hata kujiunga
na wenzake walioweka kambi Bagamoyo na siyo kususia mazoezi pekee, kisa kikiwa
ni kutaka kumaliziwa fedha zake za usajili ambazo inadaiwa bado anadai.
Kutokana na Okwi kugoma na kutoonekana kambini, Kocha wa Yanga, Hans
van Der Pluijm alijikuta akianza kumsaka mchezaji huyo kwenye vyumba vya
wachezaji jana asubuhi baada ya kuambiwa hajafika kambini.
Baada ya kuzunguka kila chumba bila mafanikio, Pluijm akaanza
kuwauliza wachezaji kadhaa juu ya Okwi lakini wote wakasema hawajui alipo,
ndipo akaamua kumfuata rafiki wa karibu wa mchezaji huyo, Hamis Kiiza ambaye
naye ni raia wa Uganda.
Alipofika kwa Kiiza naye akampa jibu kama alilopewa na wachezaji
wengine: “Sijui Okwi alipo.”
“Kocha anahangaika sana kumtafuta Okwi na hajui yupo wapi kwani leo
asubuhi (jana) aliamka na kuanza kuwauliza wachezaji na baada ya kukosa jibu la
kuridhisha, alimfuata Kiiza lakini nako aliambulia patupu,” alisema mtoa habari
wetu.
Alipoulizwa mtu mwingine wa ndani ambaye naye yupo kambini juu ya
suala hilo, alisema: “Okwi alimwambia…(anataja jina) kuwa bado kuna malipo yake
ya usajili hawajamkamilishia, ndiyo maana ameamua kugoma kuja kambini kabisa.”
Inaelezwa kuwa Okwi bado anadai dola 40,000 (Sh milioni 64) ambazo
zilisalia katika makubaliano ya awali wakati anatua klabuni hapo mwishoni mwa
mwaka jana akitokea SC Villa ya Uganda.
Alipotafutwa Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh ambaye yupo kambini,
alisema: “Sina uwezo wowote wa kulizungumzia suala hilo ila wenye mamlaka ni katibu
mkuu na ofisa habari ambao ndiyo wasemaji wa klabu," alisema.
Okwi alipotafutwa hakupatikana kwa kuwa simu yake ya mkononi ilikuwa
ikiita bila kupokelewa na baadaye haikupatikana kabisa.
0 COMMENTS:
Post a Comment