Uongozi wa mabingwa wa soka Tanzania Bara, Azam FC, umewaita
mezani Yanga waende kufanya mazungumzo kuhusiana na wachezaji wake wawili, John
Bocco pamoja na Kipre Balou kujiunga na kikosi hicho cha Jangwani.
Bocco na Balou wameingia katika rada za Yanga kufuatia ripoti ya
aliyekuwa kocha wao, Hans van Der Pluijm kuutaka uongozi wa timu hiyo kusajili
mshambuliaji ambapo Bocco amekuwa chaguo namba moja katika klabu hiyo huku
Balou akitafutwa ili azibe pengo lililoachwa na Frank Domayo.
Bocco na Balou wote wana mikataba ya kuitumikia Azam kwa miaka
mitatu inayokuja, hivyo kama Yanga itakuwa inawahitaji wachezaji hao, inabidi ivunje
mikataba yao.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Msemaji wa Azam FC, Jaffari Idd,
alisema wamesikia kuwa Yanga inawataka wachezaji wao hao, akasisitiza kuwa wao hawana
pingamizi lolote na wanawaita mezani kufanya mazungumzo kama watakuwa tayari
kuvunja mikataba waliyonayo.
“Hatuwezi kuwazuia Yanga kuwataka wachezaji wetu na tunawaambia
waje tufanye mazungumzo na kama wapo tayari kuvunja mikataba ya wachezaji hao
tutakuwa radhi kuwaruhusu,” alisema Idd.
0 COMMENTS:
Post a Comment