Mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Sekilojo Chambua, amesema kama
kikosi cha Wanajangwani hao kinataka kurejea kwenye makali yake msimu ujao, ni
lazima kisajili wachezaji watano wa safu za kiungo, beki na ushambuliaji.
Yanga msimu huu ilishindwa kutetea kombe lake la Ligi Kuu Bara
baada ya Azam kufanikiwa kulitwaa kwa mara ya kwanza tangu ilipopanda ligi kuu
mwaka 2007.
Chambua alisema tatizo kubwa ambalo liliikumba Yanga na inatakiwa
kufanya marekebisho, ni katika safu ya ulinzi wa kati ambapo wanahitajika
mabeki wawili.
Alisema pia kiungo anatakiwa atafutwe mmoja mwenye uwezo mkubwa na
mzoefu kwa kuwa kasi ya Nizar Khalfan imepungua nguvu kutokana na umri kuwa
mkubwa.
Katika safu ya ushambuliaji, wanahitajika watu wawili wa kuziba
pengo la Didier Kavumbagu aliyetimkia Azam na Emmanuel Okwi, kwani hana uhakika
kama ataendelea kuwepo kikosini hapo, hivyo atafutwe mshambuliaji mwenye uwezo
kama wake.
“Kuna matatizo madogo-madogo lakini ni lazima wafanye usajili
kwenye safu ya ulinzi, wanahitajika wachezaji wawili, kiungo mmoja na
washambuliaji wawili wa kuziba pengo la Kavumbagu na Okwi, ni vizuri kocha
akakaa na viongozi ili watafute straika mzuri mwenye uchu wa mabao! Wakifanya
hivyo nafikiri msimu ujao watatisha,” alisema Chambua.
0 COMMENTS:
Post a Comment