May 23, 2014



UCHAGUZI wa Simba umepamba moto, kila mdau ndani ya klabu hiyo lakini hata wadau wengine kwenye mchezo wa soka nchini wana hamu ya kutaka kujua kuwa nani atakuwa rais wa kwanza wa Simba.


Kwa mara ya kwanza kiongozi wa juu atakayepatikana atatumia cheo cha rais tofauti na hapo awali alikuwa akitumia kile cha mwenyekiti na msaidizi wake makamu mwenyekiti wakati wa sasa atajulikana kama makamu wa rais.
Bado suala la majina ya vyeo linaweza lisiwe kubwa sana kwa wanachama hao, lakini wanachotaka kuona ni kiongozi bora ambaye ataiongoza timu hiyo kutoka kwenye kipindi kigumu cha kuwa timu mambo yake yaliyokwenda shaghalabaghala.
Kila mmoja anajua, sasa si siri tena kwamba wakati wa Ismail Aden Rage, Simba imeporomoka kwa kiasi kikubwa licha ya kwamba klabu iliingiza fedha nyingi kupitia kwa wadhamini na hata mapato mazuri.
Kipindi ambacho Simba ilifeli kimipango, uongozi haukuwa na ubunifu, haukuwa na umakini ndiyo maana hadi leo fedha za mauzo ya Emmanuel Okwi dola 300,000 (Sh milioni 480), Simba hawajaambulia hata senti zaidi ya stori na ahadi za mwenyekiti wao anayemaliza muda wake.
Hakuna Mwanasimba atataka yatokee tena yale ya katika kipindi cha Rage, maana ndiyo wakati mgumu zaidi katika kipindi cha zaidi ya miaka kumi. Kipindi cha manyanyaso na mambo kwenda kwa kubahatisha.
Lakini wakati mchakato wa uchaguzi ukianza kuchukua hatua, Rage amekuwa akijitokeza na kuonyesha wazi anapiga debe, ameonyesha anamtetea mgombea mmoja, kitu ambacho si kizuri pia ni dalili za kuingilia kazi za kamati ya uchaguzi ambayo inapaswa kuwa huru.
Nilisikia baadhi ya wanachama wamekuwa wakisema hivi, hakuna sababu ya kuenguliwa kwa mgombea na badala yake kamati iache kila mtu akapambane kwa kura. Hilo ni wazo zuri, lakini wanaosema niliona hawakutafakari kwa kuwa sheria zinafuata mkondo.
Kamati haina uwezo wa kumkatia mtu rufaa, badala yake inazishughulikia rufaa zilizokatwa na wanachama. Vema wawashauri wale wanaotaka kukata rufaa wasifanye hivyo na si kuiambia kamati iache kufanya hivyo!
Lakini ajabu, Rage naye amekaririwa na gazeti la Tanzania Daima la jana akimtetea mgombea wa Urais Simba, Michael Wambura kwamba hakuwahi kufukuzwa Simba au hata tatizo lolote. Hiyo si kazi yake sasa, aiachie kamati.
Kamati ya uchaguzi ya Simba inaongozwa na Dokta Damas Daniel Ndumbaro ambaye ni mmoja wanasheria mahiri, maarufu nchini. Ni mwalimu wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM) ambako anafundisha sheria, pia mwalimu katika Chuo Kikuu Huria cha Dar es Salaam, pia aliwahi kuwa wakala wa kuuza wachezaji anayetambuliwa na Fifa.
Sasa vipi Ndumbaro ashindwe kuwa makini na maneno, maana yangu kitu ambacho si sahihi au sahihi kuhusiana na tuhuma kuhusu Wambura au mgombea yeyote aliyekatiwa rufaa atashindwa kung’amua vipi? Bado kamati hiyo ina wanasheria na watu wengine makini. Tatizo la Rage kuanza kuzungumzia mambo ambayo kama yakitokea yataamuliwa na kamati ni lipi?
Rage anyamaze, aache kamati ifanye kazi yake kwa uhuru bila ya kubugudhiwa kwa kuwa ina wanasheria wa kutosha ambao wanajua kipi cha kufanya. Hakuna anayeweza kumuonea Wambura kwa kuwa kila kitu kiko wazi, ikitokea kaonewa, watu wataona na kuna vyombo vinaweza kulitatua hilo kwa mujibu wa kanuni na sheria lakini mwenyekiti kuwahi na mapema kuonekana ukitetea au kutaka kuifumba kamati mdomo!
Kamati iachwe iwe huru, ili ifanye kazi yake bila ya mashinikizo. Lakini pendekezo kwa mwenyekiti wa kamati na wajumbe wake, lazima wachukue uamuzi ambao hautakuwa unammyima haki mtu yoyote. Wanachoona sahihi ndiyo wapiti hicho bila ya kujali Rage alizungumza hivi, au fulani anafanya vile. Haki ndiyo itaisaidia Simba, kuonea au kukandamazi, kutasababisha Simba iendelee kukandamizwa kama ilivyokuwa miaka minne iliyopita.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic