RAHA ya soka ni uwanjani, lakini ili
kuwe na soka la kuvutia, klabu na wadau lazima wakubali kugharamika.
Hapa nyumbani bado fedha nyingi
haziendi kwa wachezaji, badala yake wale wenye maneno mengi wanaojiita
viongozi. Wanataka kujitajirisha wao, lakini angalia wachezaji wanavyoingiza
mamilioni mfano katika Ligi Kuu England.
Manchester United imeshika nafasi ya
saba, lakini katika listi ya wachezaji 10 wanaoingiza fedha nyingi zaidi kwa
msimu ina wachezaji watatu, wawili wakiwa kwenye 5 bora.
Ukiachana na Man United, kikosi cha
bilionea wa Kirusi, Roman Abramovich cha Chelsea, kina wachezaji wanne kwenye 10
bora, huku mabingwa Manchester City inayomilikiwa na tajiri wa Kiarabu ikifunga
kwa kuwa na wachezaji wengine watatu.
Arsenal na Liverpool hazilipi sana
kiasi cha kuwafikia vigogo hao. Wafuatao ni wachezaji 10 walioingiza fedha
nyingi zaidi katika msimu uliopita wa 2013-14 zaidi kupitia malipo ya timu zao
na wadhamini.
1.
Wayne Rooney
Kifedha kwa wenyeji na wageni, huyu
ndiye ‘The Boss’, Manchester United imeishia nafasi ya saba, lakini yeye
akaonyesha kiwango zaidi na ndiye anachota mshahara mnono zaidi Premiership,
pauni 250,000 (Sh milioni 600), kwa wiki, mwisho wa msimu, ameingiza pauni
milioni 45 (zaidi ya Sh bilioni 90)!
Lakini kuna wadhamini wanaomsaidia
kutanua salio lake benki, mfano Nike pamoja na kampuni ya HarperCollins, ndiye
kinara wa mapato Ligi Kuu England kwa wachezaji.
2.
Samuel Eto'o
Huyu ndiye mchezaji tajiri zaidi
kuliko kwa wageni wanaocheza England. Raia wa Cameroon, Mwafrika tajiri Ligi
Kuu England, maana kwa msimu anaingiza pauni milioni 39 (zaidi ya Sh 80).
Alitua Chelsea, Agosti mwaka jana
akitokea Anzhi Makhachkala ya Urusi. Ingawa amekuwa hana uhakika asilimia mia
katika kikosi cha Jose Mourinho, lakini ‘shemeji’ kwa mambo ya fedha, ndiyo
mwenyewe.
3.
Rio Ferdinand
Muite babu au vyovyote, lakini
kupitia Manchester United msimu uliopita, amechota pauni milioni 37 kwa msimu
na tayari United imeachana naye.
Lakini bado anaendelea kuingiza fedha
nyingi kupitia lebo ya mavazi ya #5 anayoimiliki. Pamoja na kuondoka United,
salio lake benki, linatisha.
4.
Frank Lampard
Ana miaka 35, anaingiza pauni milioni
31 kwa msimu, akiongeza mkataba Chelsea hautazidi mwaka maana Kocha Jose
Mourinho anasisitiza anayezidi miaka 30, basi mkataba si zaidi ya muda huo.
Lakini ni kati ya wachezaji matajiri,
pauni milioni 31 kwa msimu si kitu kidogo, imemsukuma hadi nafasi ya nne.
5.
John Terry
Kati ya mabeki wanaokula mkwanja wa
juu, Chelsea inamlipa pauni 150,000, alisaini mkataba wa miaka mitano mwaka 2009.
Ingawa mkataba wake unaisha mwishoni mwa mwaka huu, umembeba kwa kiasi kikubwa
hadi 5 Bora ya wanaolipwa vizuri na wanaopata fedha nyingi kwa msimu, maana
anaingiza pauni milioni 29.
6.
Steven Gerrard
Kati ya wakongwe
waliong’ara, miaka 35 lakini bado ana miguu yenye ‘macho’. Anaingiza pauni
milioni 29 kwa msimu. Kakosa kombe, lakini uwezo uko juu, pamoja na mshahara
mzuri, lakini Adidas nao wanampa jeuri zaidi ya fedha.
7.
Ryan Giggs
Ndiye mtu mzima mwenye mkwanja zaidi,
kwa msimu anaingiza pauni milioni 27. Amemaliza msimu akiwa mchezaji mwenye
umri wa miaka 40, sasa anachukua nafasi ya kocha msaidizi chini ya Luis van
Gaal.
8.
Fernando Torres
Ndiye mchezaji ghali
zaidi Premiership kwa maana ya uhamisho wa ndani kwa ndani, alichukua fungu
lake, likamuinua kwa kipato. Lakini mshahara wake wa pauni milioni 26 kwa mwaka
unampa ‘kiburi’ cha kushika nafasi ya nane.
9.
Yaya Toure
Mwafrika wa pili kuingia kwenye 10 bora,
anachukua pauni milioni 25 kwa mwaka kutokana na mshahara wake wa pauni 200,000
kwa wiki, moja ya mishahara ya juu kabisa. Anakusanya fedha nyingi kutoka
katika malipo kutoka Kampuni ya Puma.
10.
Sergio Aguero
Mshambuliaji Muargentina ambaye
anakamilisha 10 bora na kuwa mmoja wa wachezaji wanne wageni England wanaolipwa
zaidi.
Kwa msimu mmoja anakadiriwa kuingiza
kitita cha pauni milioni 24 kutokana na mshahara wake anaopokea Man City, pia
wadhamini wake wa Puma.
IMEANDALIWA NA SALEH ALLY WA GAZETI LA CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment