CHELSEA iko
katika hatua za mwisho kuingiza benki kitita cha pauni milioni 50 (Sh120) kwa
ajili ya mauzo ya beki wake David Luiz raia wa Brazil.
Luiz ni kati
ya mabeki na viungo bora wa ulinzi, amekuwa na mafanikio makubwa katika kikosi
cha Chelsea na amewasaidia sana na kufanya kazi yake kwa ufasaha.
Kutokana na
kuonyesha uwezo, klabu inayomilikiwa na milionea wa Kiarabu ya Paris Saint
German imeamua kuonyesha nia yake ya kumnasa na mambo yameenda safi, kweli
inatoa kitita cha pauni milioni 50.
Klabu hiyo
ya Ufaransa maarufu kama PSG imekubali kutoa fedha hizo ambazo zitakuwa nyingi
zaidi kumsajili beki katika historia ya soka duniani. Kama unakumbuka Chelsea
ilimnunua Fernando Torres kwa kitita kama hicho kutoka Liverpool.
Hadi leo
pauni milioni 50 ndiyo uhamisho ghali zaidi kwenye Ligi Kuu England, maarufu
kama Premiership, lakini leo Chelsea inarudisha fedha zake kupitia beki, kitu
ambacho kinaonyesha wako makini na biashara.
Biashara
inayohusika na soka ni kubwa sana na kama inazidiwa basi na vitu vichache sana
kama madini, mafuta na kadhalika. Lakini mchezo wa soka ni biashara inayoweza
kuingiza fedha nyingi katika kipindi kifupi sana.
Angalia
Taifa Stars inapokuwa inacheza au mechi za kimataifa zinazozihusisha Yanga na
Simba, mapato yanakuwa hadi kuzidi Sh milioni 500 katika kipindi cha dakika 90,
biashara ipi inaweza kitita kama hicho ambacho kwa makadirio ya kawaida lazima
kiwe zaidi kwa kuwa lazima wajanja wachache wawe wamechota vyao tayari.
Nimeanza na
mfano wa Chelsea lakini lengo lilikuwa ni kutaka kuwaonyesha na baadaye
kuwakumbusha Simba na Yanga ambao wamefunga msimu wakiwa katika nafasi ya nne
na pili lakini wote wakiwa wamepata hasara kutokana na kutokuwa na mipango
madhubuti ya mauzo.
Simba
wamepata hasara kwa Emmanuel Okwi, walimuuza Etoile du Sahel kwa dola 300,000
(zaidi ya Sh milioni 480), lakini hadi leo ni hadithi. Wakamuachia Shomari
Kapombe aende AS Cannes ya Ufaransa, kwamba akiuzwa watapata fedha, lakini leo
wameambulia ziro. Suala la Okwi linaweza kuwa tofauti na kesi hii, ingawa kwa
kuwa Simba haijapata kitu, bado tunabaki humuhumu kwamba viongozi hawako makini
hata wanapofanikiwa kuuza wachezaji ‘bure’.
Halikadhalika
Yanga, nao mwisho wamemuacha mchezaji kama Frank Domayo akijiunga Azam FC kwa
dau kubwa la Sh milioni 70 kama ilivyoelezwa, lakini wao wameambulia patupu.
Hata kwa
wale wanaosema mwache Didier Kavumbagu aende, pia hawaangalii kwamba ni hasara
kwa Yanga kumuacha aende bila ya yenyewe kupata angalau Sh milioni 25 wakati
wenyewe walitoa fedha kumpata.
Hakuna
kiongozi mwenye hesabu ya kujua klabu imetumia kiasi gani kuwalea wachezaji
hao, lakini hata kuwapa nafasi waitumikie klabu, waonekane, bado klabu
inatakiwa kupata faida unapofikia wakati wanaondoka.
Kwa
wachezaji wenye umri mkubwa, kuwaachia waende bure bila ya kupata lolote
ingekuwa si tatizo sana, lakini si kwa Okwi, Kapombe, Kavumbagu na Domayo
ambayo bado wana uwezo wa kucheza kuanzia miaka minne hadi kumi ijayo.
Hii
inaonyesha hakuna hesabu za uhakika kwa viongozi hasa katika suala la
kuwasainisha mikataba mipya mapema kila wanapoona wamekaribia kumaliza.
Kuwaacha hadi ibaki miezi sita ni sawa na kwenda kulala na kuacha mlango wa
duka lako ukiwa wazi ukitaka wateja waone bidhaa unazouza, wakati unawapa
nafasi ya kujichagulia na kuchukua wanachotaka bila ya kufanya malipo!
Mkiachana na
kupeleka mambo kishabiki, basi kuna kila sababu ya kujifunza na kuangalia
kilichotokea kama funzo ingawa kwa Simba ambao walimuuza Okwi, wenyewe
tutaendelea kusubiri malipo!
0 COMMENTS:
Post a Comment