May 7, 2014

FULHAM



Na Saleh Ally
HAKUNA lolote wanaloweza kufanya Cardiff kwa ajili ya kuokoa nafasi yao ili kuendelea kubaki kwenye Ligi Kuu England, uhakika wamerejea daraja la kwanza.

Kinachoumiza kwa kikosi hicho, kinarejea Ligi Daraja la Kwanza ambako kilikuwa bingwa na kupanda Premiership ambayo kimeifaidi kwa msimu mmoja tu.
Wengine ambao wanarejea daraja la kwanza ni Fulham, hakuna ubishi tena kwa kuwa safari ndiyo imewakuta, angalau kidogo Norwich City wanaweza kuwa na nguvu ya kubaki lakini kwa asilimia 35 tu.
Suluhu na Chelsea katika mechi yao ya mwisho ndiyo imebaki matumaini kwamba wanaweza kubaki Premiership lakini kama Sunderland watateleza katika mechi zao mbili zilizobaki, ikishindikana basi wanaungana na Fulham na Cardiff kusema: “Kwaheri ya kuonana”.
Suala la kuteremka daraja linaendana na mambo mengi sana, lakini tafsiri yake ni kufeli. Hakuna mchezaji, kocha au kiongozi anayetaka kufeli, hivyo ni maumivu ya moyo kupita kiasi.
Lakini hata kwa mashabiki, kwa kuwa wanajijua ni sehemu ya maisha ya timu, hawapendi kuona inafeli maana wanajiona pia ni sehemu ya waliofeli, ndiyo maana wenye mapenzi ya dhati kama wale wa Fulham wanashindwa kujizuia na kuangua kilio hadharani. Inauma!

Cardiff:
Juhudi za kubaki zimeshindikana, pointi 30 ni chache sana na hata kama wakishinda mechi yao ya mwisho dhidi ya Chelsea watakuwa na 33 ambazo hazitabadilisha lolote.
Juhudi za kumtwaa Ole Gunnar  Solskjaer  hazikuzaa matunda, hazikuwa na msaada lakini kichekesho cha mambo ya soka, wapo mashabiki wao wameshikilia msimamo kuwa jezi nyekundu ndiyo zimewateremsha daraja.
Mashabiki hao waliwahi kuandamana wakitaka uamuzi wa mmiliki mpya wa timu hiyo, Vincent Tan, raia wa Thailand kutaka jezi ziwe nyekundu badala ya zile za bluu ubadilishwe, lakini ikashindikana na sasa wanasema yeye ndiye chanzo na ameishusha timu na rangi zake nyekundu!
Nafasi                                  P         W     D       L        GF    GA    PTS
20        Cardiff City         37          7      9       21     31     72     30

Fulham:
Nayo iliuzwa kama ilivyokuwa kwa Cardiff, mmiliki wake wa siku nyingi, Mohammed Al Fayed, aliamua kuachana na biashara ya mpira akamuuzia Shahid Khan.
Kumtimua Martin Jol ambaye alionekana jahazi limemshinda na kumchukua Felix Magath bado haikusaidia lolote na mwisho Fulham inayotumia uwanja mkongwe zaidi wa Craven Cottage ambao ndiyo mkongwe zaidi katika Premiership imekubali kurejea daraja la kwanza.
Fulham ni kongwe kweli, ilianzishwa mwaka 1879, sasa ina pointi 31, ikishinda mechi ya mwisho dhidi ya Crystal Palace bado ni kazi bure kwa kuwa Sunderland wameishazivuka, hivyo suala la kushuka halina mjadala na hali ya majonzi ilionekana baada ya kushindwa kujikomboa katika mechi yao ya mwisho, mashabiki wakaangua vilio.
Nafasi                               P            W     D       L        GF    GA    PTS
19     Fulham                37   9       4       24     38     83     31    


Norwich City:
Kocha Neil Adams anaichukulia mechi yao dhidi ya Arsenal Mei 11 wakiwa nyumbani ndiyo jibu la mwisho kwa kuwa watakuwa nyumbani. Wakishinda watafikisha pointi 36 na Sunderland wana 35, lakini wana mechi mbili mkononi.
Hivyo Norwich wana kazi mbili, kwanza kuhakikisha wanaifunga Arsenal ambayo msimu uliopita waliifunga Wigan katika mechi ya mwisho na kuiteremsha daraja.
Kazi ya pili kwa Norwich ni kurudi nyumbani na kufanya maombi ya kumuombea adui njaa. Lazima waombe Sunderland ipoteze mechi zake zote mbili zilizobaki dhidi ya Wes Brom na Swansea na zote watakuwa nyumbani!
Kama watashuka, ndiyo itakuwa timu yenye nahodha Mwafrika kushuka kutoka Premiership msimu huu maana inaongozwa na Mcameroon, Sebastien Bassong.

Nafasi                                P W     D       L        GF    GA    PTS
 18    Norwich City      37   8       9       20     28     60     33
         

 Fin.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic