May 19, 2014

LUIZ NA SILVA


PREMIER LEAGUE inaendelea kuwa ligi yenye mvuto zaidi dunia kwa wapenda soka kutokana na mengi.
Uwanjani ni jambo la kwanza, lakini mavazi, gumzo na hata namna timu zinazotoa fedha kuwanasa wachezaji.
Angalia namna wachezaji ghali walivyofanikiwa, wako waliofeli kutokana na timu zao kufanya vibaya baada ya msimu wa 2013-14.
Lakini wako wameonyesha matunda na timu haziwezi kujuta kutokana na kutoa mamilioni ya pauni kuwanasa.
OZIL
Wako walisajiliwa zaidi ya miaka mitano iliyopita wameendelea kubaki juu kwa kuwa usajili wao haujapitwa na wengi au hata mmoja.
Ukipiga hesabu, utagundua kweli mamilioni yanatumika kwenye soka na England sasa wamekuwa wakionyesha ni ligi yenye fedha, kikosi hiki unaweza kukiita kikosi cha mamilioni.

De Gea:
David de Gea ndiye kipa ghali zaidi wa Premiership kutokana na dau la pauni milioni 17.5 (Sh bilioni 45.5) ambazo Man United, walitoa kwa Atletico Madrid  mwaka 2011 kumnasa.
Amefanya kazi kubwa msimu uliopita, lakini hakuambulia kombe lolote kutokana na kikosi chake kukwama kwenye nafasi ya saba kwa zaidi ya miezi miwili, hadi mwisho wa ligi.
Rio:
Pamoja na ukongwe wake, alicheza mechi chini ya kumi za Premiership msimu uliopita, lakini amemaliza akiwa mmoja wa mabeki ghali.
Aliweka rekodi ya kuwa beki ghali zaidi England alipojiunga na Man United, mwaka 2002 akitokea Leeds. Ameendelea kutesa na rekodi yake hiyo kwani hakuna aliyevuka pauni milioni 30 (Sh bilioni 78) alizonunuliwa, tayari amekubali na kuondoka Man United ambayo haikuambulia lolote msimu huu.
Luiz:
David Luiz hakuwa chaguo la kwanza la Jose Mourinho lakini uwezo wake uko juu na sehemu ya tegemeo la timu ya taifa ya Brazil kwenye Kombe la Dunia.
Alisajiliwa kwa pauni milioni 26.5 (Sh bilioni 69) akitokea Benfica, ni kati ya uhamisho wa juu England kwa upande wa mabeki, lakini msimu huu wametoka kapa kwa kuwa Chelsea ya Mourinho haikupata hata kikombe cha ‘chai’.

Lescott:
Joleon Lescott ni kati ya mabeki ambao hawakuwa na nafasi kubwa sana, lakini walifanya vema kila walipoipata nafasi hiyo katika kikosi cha Manuel Pellegrini.
Angalau yuko kwenye kikosi kilichobeba ubingwa wa England msimu huu. Manchester City ilitoa pauni milioni 24 mwaka 2009 kumpata akitokea Everton.
Fernandinho:
Mkurugenzi wa masuala ya ufundi ya Barcelona, Txiki Begiristain alikubali kulipa pauni milioni 35 (Sh bilioni 91) kwa Shakhtar Donetsk ili kumpata kiungo huyo Mbrazili, lakini Man City wakapanda dau na kutoa pauni milioni 39.5 (Sh bilioni 102) na kumtwaa.
Kwa mujibu wa watalaamu, ndiye alikuwa chagizo kubwa la mabadiliko ya uchezaji wa Man City kutokana na uwezo mkubwa wa kukaba, kuchezesha timu na mwisho kufunga.
Mata:
Manchester United ililazimika kukubali kuilipa Chelsea dau kubwa la pauni milioni 39 (Sh bilioni 101) ili kumpata Juan Mata, tena alikaribishwa baada ya kutua na chopa.
Mwisho mambo hayakuwa mazuri ingawa hakuna anayeweza kusema ana hofu kutokana na uwezo wake, alioonyesha anaweza.
Kitu kibaya kwake, hatacheza michuano yoyote ya kimataifa msimu ujao kwa ngazi ya klabu kwa kuwa Man United, imekwama nafasi ya saba.
Hazard:
Alishuka kidogo katika mechi kumi za mwisho, lakini ndiye alikuwa chachu ya ushindi ya Chelsea ambayo ilikubali kutoboka mifuko na kutoa pauni milioni 35 (Sh bilioni 91) na kuipa Lille ya Ufaransa mwaka 2012 ili kumnasa.
Kamwe Chelsea haiwezi kujuta kwa Mbelgiji huyo kutokana na uwezo mkubwa ambao amekuwa akiuonyesha hata kama haitakuwa imebeba kombe.
Ozil:
Mjerumani mwenye asili ya Uturuki, ndiye anashikilia usajili ghali zaidi England msimu huu. Arsenal ambayo kocha wake, Arsene Wenger alikuwa anasifika kwa ubahili alikubali kutoa pauni milioni 42.5 (Sh bilioni 110) ili ampate.
Ingawa hakufikia usajili wa Fernando Torres wa pauni milioni 50 (Sh bilioni 130) msimu mmoja kabla, lakini alionyesha kuwa anaweza kubadilika na kusajili ghali.
Ozil ambaye alitokea Real Madrid ana cha kujivunia na kuonyesha hakukosea kutua Arsenal kwa kuwa wamekuwa mabingwa wa Kombe la FA.
Rooney:
Ingawa alitua Manchester United mwaka 2004 akitokea Everton, bado uhamisho wake wa pauni milioni 30 (Sh bilioni 78) uko juu pia.
Man United haiwezi kujuta, Rooney amekuwa na faida, amekuwa msaada mkubwa katika kikosi hicho licha ya kwamba msimu huu kilifeli vibaya.
Juhudi za kumbakiza zilifanyika kuepuka Mourinho kumnasa, na ndiye amekuwa tegemeo zaidi United kwa kipindi cha misimu minne sasa.

Aguero:
Kun Aguero, raia wa Argentina mwenye uwezo mkubwa lakini amekuwa akisumbuka sana kwa majeraha. Manchester City ilimwaga pauni milioni 39.5 (Sh bilioni 102) kumpata kutoka Atletico Madrid ya Hispania, hiyo ilikuwa mwaka 2011.
Amekuwa msaada mkubwa kwa City, miaka miwili iliyopita alifunga bao katika mechi ya mwisho City ikibeba ubingwa chini ya Roberto Mancini na msimu huu amefunga pia bao katika mechi ya mwisho na City ikabeba tena ubingwa.
Torres:
Fernando Torres, amefeli kuwaridhisha mashabiki, lakini amechukua Kombe la Ligi ya Mabingwa na mengi akiwa na Chelsea baada ya kununuliwa kwa kitita cha pauni milioni 50 akitokea Liverpool mwaka 2011.
Bado ana uwezo, huenda anatakiwa kutulia au kukubali kuondoka Chelsea, lakini si mchezaji wa kusema amekwisha au hajiwezi. Uhamisho wake ndiyo ghali zaidi ndani ya England.
Kwa hesabu inaonekana Man City na Chelsea ndiyo timu ambazo zimekuwa zikimwaga fedha nyingi kupata wachezaji.
Timu hizo, moja imekuwa bingwa na nyingine imeshika nafasi ya tatu. Inawezekana kukawa na presha kwa Mourinho, lakini bado ana nafasi ya kufanya vema msimu ujao.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic