May 19, 2014



Na Saleh Ally
ANGALIA mashabiki wa Arsenal wanavyotembea leo kifua mbele, kila mmoja anafurahia na kuonyesha kuwa ameshinda kitu kikubwa ikiwa ni siku moja tu baada ya klabu hiyo maarufu kuweka kwenye kabati kombe jingine la FA.

Arsenal ina kikosi kizuri, kinachocheza soka la kuvutia, huenda kuliko kingine chochote nchini England. Soka lao linavutia, linapangika na raha kuangalia wakiwa wanacheza.

Ukizungumzia uchumi, Arsenal iko juu kwa kuwa imekuwa ikishika nafasi ya nne na tano (inacheza hapo) kwa utajiri duniani kote baada ya magwiji kama Real Madrid, Manchester United, Barcelona na Bayern Munich.
Lakini kilichokuwa kinawakera wengi ni kuona Arsenal inashindwa kupata angalau kombe moja la Ligi Kuu England tokea msimu wa 2003-04. Lakini ilishindwa kuchukua kombe lolote la FA tokea mwaka 2005.

Arsenal walichoka na hasa mashabiki, hawakutaka tena kusikia taarifa za soka la kuvutia wala uchumi mzuri. Walichotaka ni makombe na uvumilivu wao ulikuwa ni miaka mitano tu na ilipovuka 2010, wakabadilika na kuwa mbogo.
Mzigo wote ukaangushiwa kwa Arsene Wenger, kocha aliyetua Arsenal mwaka 1996 akitokea Grampus Eight ya Japan ikiwa ni miaka 10 baada ya Alex Chapman Ferguson kujiunga na Manchester United.
Baada ya hapo, Wenger amekuwa ni kocha mwenye mafanikio makubwa sana na Arsenal lakini kizazi cha kuanzia 2005 kimekuwa kikiona hajafanya lolote kwa kuwa hakuwa amechukua kombe kwa siku 3,283 au unaweza kusema miaka tisa.
Siku hizo 3,283 zimekuwa ni zenye mateso makubwa kwa Wenger ambaye ameambulia dharau kupindukia, huku baadhi wakiingia na mabango uwanjani wakimbeza kwa maneno lukuki yakiwemo yale kuwa ndiye kocha mbahili kuliko wote duniani.
Wengine walimueleza kama anataka masuala ya uchumi anaweza kwenda kufanya kazi benki kuu ya Ufaransa au ikishindikana akawe mshauri wa uchumi wa Waziri Mkuu wa Uingereza wakati huo Tony Blair. Lakini hakuwahi kushusha silaha, alipambana bila ya kuchoka, kitu ambacho ni funzo kubwa.
Kuanzia mwaka 2011, mambo yalizidi kuonekana magumu zaidi kwa Wenger, alizidi kupoteza uelekeo na ule uvumilivu wake ulionekana kuanza kupotea taratibu na hata ile hali yake ya utulivu ilizidi kupotea.
Wazi alionekana hayuko vizuri, hakuwa na furaha tena na ilionyesha kiasi gani anaumia kwani Arsenal ndiyo imekuwa timu inayoongoza kukaa kileleni mwa Premier League kwa misimu miwili sasa, lakini ikifikia mwishoni mwa ligi inaporomoka.
Lakini mwisho amewaziba midomo wote waliokuwa wakimtupia dharau, waliosahau ubora wake na hata Kombe la FA wanalolifurahia tayari alikuwa amelibeba mara nne, hili la sasa ni la tano, hivyo si kitu kigeni sana.
Ukitaka kujua mpira hauna shukurani, angalia mashabiki wanavyofurahia leo utadhani wameshinda wao walikuwa na mipango au waliandaa timu. Uwezo wa mashabiki wa soka duniani kote ni kushangilia na kulaumu, sasa lawama kwisha.
Kocha:
Amekuwa kocha mkuu tokea mwaka 1984 alipokuwa akiinoa Nancy-Lorraine ambayo aliiacha mwaka 1987 na kujiunga na AS Monaco.
Monaco nayo aliiacha mwaka 1994 na mwaka uliofuatia akajiunga na na Nagpya Grampus Eight ya Japan aliyokaa nayo hadi 1996 alipoondoka nchini humo na kutua London, England na kuanza kazi Arsenal.
Kwa miaka 30, Wenger amefundisha timu nne tu, hii ni sehemu ya kuonyesha si kocha wa kuyumba, mwenye tamaa au mwenye haraka.
Pia inathibitisha Wenger si mtu mwenye haraka badala yake ni mvumilivu ambaye yuko tayari kutimiza malengo yake zaidi kuliko kuhofia maneno-maneno.
Wenger ni kati ya makocha bora na wenye mafanikio ya juu sana duniani kwa ushindi wa timu na mafanikio binafsi.
Tayari amesema hana mpango wa kuondoka Arsenal, anataka kuendelea kubaki na kurekebisha mambo. Huenda atarejea msimu ujao na kufanya makubwa zaidi kwa kurekebisha makosa kwenye Premiership.

MAKOMBE:
AKIWA NA KLABU
Monaco (Ufaransa)
                    Ubingwa wa Ufaransa (1987–88)
                    Kombe la Ufaransa (1990–91)

Nagoya (Japan)
                    Kombe la Emperor (1995)
                    J-League Super Cup (1996)
                   
Arsenal (England)
                    Premier League (1997–98, 2001–02, 2003–04)
                    FA Cup(1997–98, 2001–02, 2002–03, 2004–05, 2013–14)
                    Ngao ya Jamii (1998, 1999, 2002, 2004)

TUZO:
BINAFSI:
                    Kocha wa Mwaka Ufaransa (2008)
                    Kocha wa Mwaka wa Ligi ya Japan (1995)
                    Meneja Bora Premier League (1998, 2002, 2004)
                    Kocha Bora wa LMA (2001–02, 2003–04)
                    Kocha Bora wa BBC (2002, 2004)
                    Kocha wa Mwezi Premier League (mataji 13 tokea Machi 1998 hadi Septemba 2013)
                    Kocha Bora wa Dunia wa Muongo (miaka 10) 2001–2010

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic