RIVALDO alifanikiwa kushinda Tuzo
ya Mchezaji Bora wa Ulaya, mara tu baada ya mafanikio hayo akaamua kuanika
hisia zake na kumwambia kocha wake kwamba hatacheza tena upande wa kushoto,
yaani winga. Badala yake anataka kucheza namba kumi.
Kocha wake katika kikosi cha Barcelona wakati huo akamuambia sawa,
wakati unachukua tuzo ya mchezaji bora ulikuwa unacheza kama winga wa kushoto,
sasa umevimba kichwa, utakula jeuri yako. Rivaldo akaanza kusota benchi, hadi
aliposalimu amri na kukubali kucheza winga ya kushoto.
Kocha huyo alikuwa ni Luis van
Gaal, bosi mpya wa Manchester United ambaye anaaminika anafanana na Alex
Ferguson kiutendaji na hasa namna ya kufanya kazi na mastaa wakubwa.
Van Gaal aliyekuwa Kocha Bora wa
Dunia mwaka 1995 si mtu wa kubabaika, anaijua kazi yake, pia ni mwenye msimamo
wa anachotaka, lakini anavutiwa kuwa na urafiki na wachezaji wake.
Kikubwa ambacho wengi wanataka
kujua ni kuhusu nini atakifanya kuibadilisha Manchester United ambayo ni mfupa
uliomshinda David Moyes baada ya Ferguson ‘kuula’ kwa raha zake, tena kwa
ulaiini.
Kushindwa hakitakuwa kitu rahisi
kwa maana ya rekodi, maana van Gaal ameshinda karibu mataji yote, ukianza na
ubingwa wa Uholanzi akiwa na Ajax, ule wa La Liga akiwa na Barcelona, pia
bingwa wa Bundesliga akiwa na Bayern Munich.
Usisahau Kombe la Washindi Ulaya
na Ligi ya Mabingwa Ulaya, hivyo hana ugeni hata kidogo na makombe, ingawa si
‘garantii’ kwamba kupitia rekodi zake leo ndiyo atashinda tena.
Kinachowaumiza kichwa wengi ni
mfumo, kawaida van Gaal ‘anaabudu’ ule wa 4-3-3 ambao utakuwa ni mpya na mgumu
kwa wachezaji wa Manchester United.
Hata sasa akiwa na kikosi cha
timu ya taifa ya Uholanzi, van Gaal amekuwa akiutumia zaidi mfumo huo kama
namna moja kwake, lakini ana tabia nyingine ya kujaribu mifumo.
Kawaida van Gaal anasema anataka
kutumia mfumo kutokana na wachezaji. Kwa Manchester United, 4-4-2 umekuwa ndiyo
mfumo mama, lakini kwake ni nadra, huenda akaujaribu pia.
Lakini amekuwa akitumia mifumo
mingine na kuwashangaza wengi, mfano wakati akiwa na Barcelona, amewahi kutumia
mfumo wa 2-3-2-3.
Manchester United wataweza mfumo
huo?
Atawatumia akina nani na
ukizingatia safu ya ulinzi imeporomoka na kwa mfumo wake lazima awe na
wachezaji wakongwe?
Hana namba sita wa uhakika,
Michael Carrick ataingia kwenye mfumo wake? Akiwa Barcelona aliwatumia zaidi wachezaji
wake wakati huo Pep Guardiola na Puyol kwenye ukabaji, anahitaji wachezaji wa
namna hiyo.
Ili kuingiza mifumo anayotaka,
van Gaal analazimika kufanya usajili hasa kwenye kiungo ambako Kroos kutoka
Bayern anamfaa, lakini beki mkongwe angalau mmoja wa kusaidiana na Chris
Smalling, John Evans na Phil Jones.
0 COMMENTS:
Post a Comment