May 21, 2014

KASSIM DEWJI (KULIA) AKIZUNGUMZA JAMBO NA HASSAN DALALI 'FIELD MARSHAL

Na Saleh Ally
KATIBU Mkuu wa zamani wa Simba, Kassim Mohammed Dewji, ana umaarufu mkubwa kutokana na kuwa na mafanikio mengi wakati akiiongoza klabu hiyo kwa nyakati tofauti.

Dewji, ‘raia’ wa Singida, amekuwa akisifika kwa fitna za kisoka, ingawa mwenyewe amekuwa akisisitiza, alichokuwa akifanya ni mipango inayoendana na uhamasishaji kama lile tukio alilodanganya kuwa amezimia.
“Nilidanganya nimezimia wakati wa mapumziko, Yanga walikuwa wanaongoza kwa bao 1-0 dhidi ya Simba. Nilipodanganya kama nimezinduka nilianza kulalamika nikawaambia wachezaji wataniua.
“Tena nilikuwa nikiwataja kwa majina, Baada ya hapo wachezaji waliona kama wangefungwa, basi kweli wangeniua. Kipindi cha pili Simba ilipata mabao mawili na mwisho tukawa tumeshinda. Sasa hizo ndizo fitna za soka na si zaidi,” anasema Dewji.
Wakati akiwa katibu mwenezi, Dewji aliisaidia Simba kubeba makombe matatu ya Ligi Kuu Bara na matatu ya Cecafa, sasa maarufu kama Kagame.
 Alipochukua nafasi ya katibu mkuu, akaiongoza kutwaa makombe mengine matatu, mawili Bara na Kagame moja, pamoja na makombe matatu ya Tusker akiwa katibu mkuu. Hii inamfanya awe kiongozi aliyeshuhudia makombe mengi zaidi ya Simba akiwa madarakani.
Pia ndiye alikuwa kiongozi wa juu wakati Simba ikiing’oa Zamalek mwaka 2003 na kuweka rekodi ya kuwa timu iliyopokelewa na watu wengi zaidi wakati imerejea nchini ikitokea Misri.
Dewji ambaye amekaa kimya kwa muda mrefu, ameibuka siku chache kabla ya uchaguzi wa Simba na kusisitiza uongozi uliopita, haukuitendea haki Simba na kusisitiza tena bila ya kutaja anaona mgombea yupi ni sahihi, kwamba wanachama wa klabu hiyo wawe makini.
Simba inakusanya zaidi ya Sh milioni 400 kutoka kwa wadhamini wa klabu na wale wa ligi ambao ni TBL, Vodacom na Azam TV. Ukijumlisha na mapato ya mlangoni, ni zaidi ya Sh milioni 800, lakini ikaishia katika nafasi ya nne.

SALEHJEMBE:  Tofauti kifedha sasa na kipindi kile ikoje?
Dewji: Ukianza kwa wadhamini wetu ambao ni MeTL walikuwa wakitoa Sh milioni 100, Twiga Cement milioni 30 na NBC milioni 30 pia. Utaona kwa fedha hizo, tulifanya mambo mengi makubwa, sasa ajabu udhamini hadi zaidi ya Sh milioni 300, lakini hakuna kitu!
Championi: Unafikiri tatizo ni nini?
Dewji: Viongozi kutokuwa na uchungu, lakini mipango ili kuhakikisha timu inafanya vizuri.
Ndiyo maana nimekuwa nikisisitiza bila ya kumtaja mtu kwamba Simba wawe makini kwenye uchaguzi, wachague viongozi wanaoingia kwa ajili ya klabu na timu, si kuongeza malumbano, migogoro na kujali matumbo yao.

SALEHJEMBE:  Simba ina majengo mawili, moja linaitwa Ghorofa la Dewji, kwa nini?
Dewji: Nililijenga wakati wa uongozi wangu, niliita mwekezaji, akalijenga na tukampa miaka saba arudishe fedha yake. Sasa leo Simba inaingiza shilingi milioni 180 kwa upande wa maduka tu. Msingi wa pale ni ghorofa nane, tukipata kiongozi imara, basi anaweza kuendeleza jengo hilo.
Nakumbuka wakati wetu, jengo lile la zamani lilikuwa linaingiza shilingi milioni 2.4 kwa mwaka. Leo Simba wana mtaji mkubwa, lakini kuna viongozi wamekuwa wakila fedha za klabu tu.

SALEHJEMBE:  Wapo wanaosema uliiba fedha nyingi ukiwa Simba, ni kweli?
Dewji: Hayo ni maneno, tena ya watu wasioitakia Simba mema. Jiulize nani leo ananishukuru kwa ubunifu na Simba inaingiza milioni 180 kila mwaka kupitia jengo nililojenga? Pale kulikuwa na makontena tu yaliyowekwa na mzee Gulum, mimi ndiye nilichukua uamuzi mgumu, kwani nani anashukuru?
Kulaumiwa ni kawaida, lakini rekodi na historia vinaonyesha nilichokifanya Simba na leo utaona ugumu ulivyo na hadhi ya Simba inazidi kuporomoka.
Vizuri wakaingia viongozi wenye uwezo, wenye timu itakayowasaidia vizuri kuijenga Simba upya na si kuendeleza matatizo na malumbano ambayo yameiporomosha klabu yetu.

SALEHJEMBE:  Kuna taarifa ulipata kashfa ya kuuza basi la Simba
Dewji: Watu hawaelewi na wamekuwa wakinichafua tu, tulitakiwa kumsajili (Mark) Sirengo kwa shilingi milioni 6 kutoka Kenya. Hatukuwa nazo, nikauza basi kwa Sh milioni nane, tukamsajili. Alipotua nchini akatusaidia kubeba Kombe la Kagame, tukapata dola 20,000. Nikatoa nusu yake nikanunua basi jipya.

SALEHJEMBE:  Katika miaka yako 25 ndani ya Simba, unakumbuka kosa gani kubwa uliwafanyia Wanasimba, leo unaweza ukawaomba wakusamehe?
Dewji: Mimi ni binadamu, kosa kubwa zaidi ni kipindi naondoka Simba mwaka 2004. Niliondoka bila ya kumuandaa kiongozi yeyote ambaye angenirithi na kuendelea kuisaidia. Badala yake, klabu ikaanza kuporomoka hadi kufikia ilivyo leo, kweli niliwakosea sana.

SALEHJEMBE: Mlifanya vizuri wakati ule wa kina Mark Sirengo na wengine. Lakini wachezaji wengi wa kigeni wa Simba hawana cheche, msimu uliopita alibaki Amissi Tambwe tu, tatizo nini?
Dewji: Suala la kupata wachezaji wa kigeni linahitaji jicho la pili, linahitaji mtu mzoefu. Sirengo alifuatwa na mmoja wa viongozi wa usajili wakati huo, sasa ni mgombea nisingependa kumtaja. Ni kati ya viongozi wanaojua mchezaji gani wa kigeni anaweza kuwa msaada.
Kikubwa ni umakini na wakati wa usajili kuangalia wachezaji si kuangalia kiongozi naye atapata kiasi gani wakati wa usajili. Lakini mimi ni muumini wa wachezaji wa nyumbani, bora kuwa na wa nyumbani kuliko wa kigeni ambao wanakaa benchi.

SALEHJEMBE:  Hauna mpango wa kurejea Simba kwa mara nyingine?
Dewji: Hakika mimi niko Simba siku zote, sihitaji kugombea tena, hivyo nitakuwa tayari kutoa msaada wowote ninaoweza kwa ajili ya kuisaidia Simba. Nawakaribisha waje.

SALEHJEMBE:  Ungependa nani ashinde katika uchaguzi wa Juni 29 ambao ndiyo unaonekana kuwa mkombozi wa Simba iliyodorora kwa miaka minne?
Dewji: Siko hapa kupiga kampeni, lakini niwe mkweli, wanachama wa Simba wawe makini, wasirubuniwe na maneno kwa kuwa bahati nzuri wanawajua karibu viongozi wote wanaogombea, hasa wale wa ngazi za juu, hakuna mgeni.
Wanajua walikotokea, wamepitia wapi na wameifanyia Simba kitu gani. Hawana sababu ya kukurupuka, wala wasikubali kulaghaiwa na maneno au ujanja wa watu ambao wanajua kabisa kuwa wamekuwa tatizo wakiwa Simba au kwenye taasisi nyingine. Wachague kiongozi sahihi au msaada sahihi kwa klabu yao.

SALEHJEMBE: Ahsante, karibu Championi.
Dewji: Nashukuru sana.



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic