Kocha wa Taifa Stars, Mart Nooij
amesema wachezaji wake wako tayari kwa ajili ya mechi ya Kombe la Afrika dhidi
ya Zimbabwe (Mighty Warriors) itakayochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari
jijini Dar es Salaam leo (Mei 16 mwaka huu), Nooij amesema kabla ya kuja
Tanzania alikuwa akifuatilia Ligi Kuu ya Vodacom (VPL), hivyo anawafahamu
wachezaji wengi.
Amesema wachezaji wanaounda kikosi
chake ni wenye uzoefu na mechi za kimataifa, hivyo wapo tayari kwa ajili ya
mechi hiyo, kwani wamepata mechi za kirafiki na mazoezi ya kutosha kwenye kambi
iliyokuwa Tukuyu mkoani Mbeya ambapo kulikuwa na utulivu mkubwa.
Nooij amesema ujio wa
washambuliaji Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wanaochezea timu ya TP Mazembe
ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (RDC) kutaongeza morali ya kikosi chake.
Samata na Ulimwengu watawasili
nchini Jumamosi mchana, saa 7.30 mchana kwa ndege ya Ethiopian Airlines
wakitokea Khartoum, Sudan ambapo leo (Mei 16 mwaka huu) wanacheza mechi ya Ligi
ya Mabingwa dhidi ya Al Hilal ya huko.
Wachezaji waliopo kambini kwa sasa
ni Deogratias Munishi, Aishi Manula, Said Moradi, Oscar Joshua, Kelvin Yondani,
Erasto Nyoni, Nadir Haroub, Shomari Kapombe, Aggrey Morris, Himid Mao, Mwinyi
Kazimoto, Frank Domayo, Amri Kiemba, Jonas Mkude, Haruna Chanongo, Simon Msuva,
Mrisho Ngasa, Khamis Mcha, Ramadhan Singano, John Bocco, Elias maguli na Kelvin
Friday.
Wakati huo huo, timu ya Zimbabwe
(Mighty Warriors) inawasili kesho alfajiri (Mei 17 mwaka huu) kwa ndege ya
Ethiopian Airlines ikiwa na msafara wa watu 27. Kesho saa 4 asubuhi (Mei 17
mwaka huu) Kocha wa timu hiyo atakuwa na mkutano na waandishi wa habari katika
ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Tiketi kwa ajili ya mechi hiyo
zinaanza kuuzwa kesho (Mei 17 mwaka huu) kwenye vituo vya Shule ya Sekondari
Benjamin Mkapa, mgahawa wa Steers uliopo Mtaa wa Ohio na Samora, OilCom Ubungo,
Uwanja wa Taifa, kituo cha mafuta Buguruni na Dar Live Mbagala. Viingilio ni
sh. 5,000, sh. 10,000 na sh. 20,000 tu.
0 COMMENTS:
Post a Comment