Kiungo wa Yanga, Omega Seme, aliyerudishwa hivi karibuni katika
klabu hiyo akitokea Prisons ya jijini Mbeya alikokuwa akicheza soka kwa mkopo,
anatarajia kutua jijini Dar es Salaam leo.
Inaelezwa kuwa kiungo huyo atakwenda klabuni moja kwa moja na
jukumu kubwa atakalopewa ni kuziba pengo lililoachwa na Frank Domayo
aliyetimkia Azam FC.
Hivi karibuni, Domayo ambaye alikuwa ni mmoja wa wachezaji wa
kiungo wa kutumainiwa wa Yanga, aliachana na klabu hiyo na kumwaga wino wa
kuitumikia Azam kwa miaka miwili, lakini haraka sana Yanga walimrudisha Seme
ili kuziba pengo lake.
Seme, msimu uliopita alitamba sana na kikosi cha Prisons
alichokuwa akikitumikia kwa mkopo, hali iliyosababisha viongozi wake kumpigia
simu na kumtaka kuja Dar es Salaam haraka.
Seme amesema ameelezwa kuwa anatakiwa kuanza haraka maandalizi kwa ajili ya msimu ujao ili awe fiti kuweza kukabiliana na mikikimikiki ya ligi msimu ujao.
Alisema atakapofika Dar es Salaam leo mchana, atakwenda moja kwa
moja makao makuu ya klabu hiyo na kukutana na uongozi wake kabla ya kwenda
nyumbani kwao.
Hata hivyo, mchezaji huyo mwenye uwezo mkubwa wa kucheza nafasi
mbalimbali uwanjani, alisema hajui ataambiwa nini na viongozi wake mara baada
ya kukutana nao lakini endapo watampatia jukumu la kuziba pengo la Domayo, yupo
tayari na ataifanyia kazi kubwa timu hiyo.
“Wakiniamini na kunipa
nafasi nitafanya kazi kubwa ambayo kila mtu ataipenda, kwani najiamini na nina
uwezo mkubwa wa kucheza soka.
“Kesho (leo), natarajia kuja Dar es Salaam kwa ajili ya kuanza
maandalizi yangu ya kujiandaa na msimu ujao wa ligi kuu,” alisema.
0 COMMENTS:
Post a Comment