UCHAGUZI Mkuu
wa Klabu ya Simba unatarajiwa kufanyika keshokutwa Jumapili, mmoja wa wagombea
katika uchaguzi huo ni Ally Suru.
Suru
anayewania nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba amezungumza na
gazeti hili na kueleza kuhusu mipango yake, ambapo kauli mbiu yake ni ‘Ushindi
Kwanza’.
Suru ambaye
ana Shahada ya Uzamili ya Fedha na Uwekezaji (MSc-Finance & Investment)
aliyoipata katika Chuo Kikuu cha Coventry, Uingereza, amewaahidi Wanasimba yafuatayo:
“Kubwa
nitakaloanza nalo baada ya kuingia madarakani, ni kuboresha timu, maana kwa muda wa miaka miwili iliyopita timu yetu
imepoteza hadhi.
“Kuimarisha timu ya vijana pia itakuwa moja
za kazi zangu kubwa, ili kupata timu bora ya wakubwa ni lazima uwekeze kwa vijana
wenye vipaji.
“Jambo jingine ni ujenzi wa kituo cha michezo
ili kuhakikisha klabu yetu inakuwa na uwanja wake, awamu ya kwanza ni ujenzi wa
uwanja wa mazoezi na hosteli, ambao ni mpango wa muda mfupi.
“Awamu ya pili ni mkakati wa ujenzi wa uwanja
wa kudumu ili kuiwezesha klabu yetu iweze kumiliki uwanja wake binafsi wa
kiwango cha kisasa.
“Lakini pia kuna umuhimu wa klabu kuwa na akaunti
mbili; ya kawaida na ya maendeleo kwani taasisi zote duniani ambazo
zimefanikiwa zimekuwa na huu utaratibu kwa kutofautisha fedha za matumizi na
zile za maendeleo.
“Kuongeza wanachama pia ni moja ya silaha za
maendeleo, rasilimali watu ni muhimu sana, mfano tukiwa na wanachama 100,000 wanaolipa
ada kwa mwaka tutaweza kukusanya jumla ya shilingi bilioni 1.2 kwa mwaka.”
Suru pia pia ana shahada nyingine ya uhasibu
kutoka Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), amewahi kuwa kiongozi wa nyadhifa
zifuatazo; Mwenyekiti wa Michezo Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi hadi
sasa, Mjumbe wa Mkutano Mkuu Shimiwi Taifa hadi sasa, Makamu Mwenyekiti wa
Michezo Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi.
0 COMMENTS:
Post a Comment