WAKATI mwingine najiuliza, hivi katika hizi klabu za soka
na hasa hizi mbili kongwe kuna nini hasa hadi inafikia watu kujengeana uadui,
uhasama tena hadharani na hata kutupiana maneno makali bila ya woga?
Ndani ya Simba sasa ni harufu ya malumbano na chuki za
wazi, lakini tafsiri ya hapa ni kila upande unataka kushika hatamu na kuingoza
klabu hiyo. Siku zote swali langu limekuwa hivi, upande mmoja ukipata madaraka
na chuki ndiyo umekuwa msingi, utaweza vipi kuongoza bila ya umoja?
Rufaa aliyowasilisha Michael Wambura ndiyo ilikuwa gumzo kubwa sana na kila mmoja alitaka kujua kama mgombea huyo aliyeenguliwa kwa mara ya pili na kamati ya uchaguzi baada ya
kubainika alifanya kampeni kabla ya muda wake, atapita, imeshindikana na ameondolewa tena.
Kamati ya rufaa ya TFF, ilianza kukaa jana mchana kujadili
kuhusiana na alichowasilisha na kile cha kamati ya uchaguzi. Lakini kuna mambo
yanashangaza kabisa!
Achana na kwamba Wambura ameishapigwa chini, lakini katika hoja tisa alizowasilisha Michael Wambura kujitetea
katika kamati ya rufaa ya TFF, moja inasisitiza uamuzi wa Rais wa Shirikisho la
Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi wa kutaka uchaguzi usimamishwe, usikilizwe!
Hapa ndiyo nachoka kabisa, kwamba kumbe Wambura anamuunga
mkono Malinzi licha ya wanachama wa Simba kuona uamuzi wa kiongozi huyo wa TFF
hauutakii klabu yao mema.
Ndiyo maana lundo la wanachama lilijitokea klabuni kwao na
kupinga hatua hiyo ya Malinzi kuwataka Simba wasimamishe uchaguzi na kuunda
kamati ya maadili, dakika 30 tu baada ya yeye kutangaza. Maswali yakawa mengi,
kwani Malinzi hakulijua hilo awali na hata kamati ya uchaguzi ya Simba
ikampinga kwamba kisheria hana mamlaka au uwezo wa kusimamisha uchaguzi.
Kusimamisha uchaguzi wa Simba ni kuiangamiza klabu hiyo
ambayo sasa inataka ahueni, inataka mabadiliko pia inahitaji watu makini ambao
watawaunganisha Wanasimba upya kwa lengo la kuijenga tofari kwa tofari.
Sasa mgombea aliyeenguliwa pia anaomba uchaguzi
usimamishwe akisistiza kilichoelezwa na Malinzi kifuatwe. Awali kwenye hili,
nilieleza kuwa sikubaliani na Malinzi. Lakini kwa mara ya kwanza nasema
hadharani kuwa napingana na hoja hiyo ya Wambura na ikiwezekana yeye pia.
Si sahihi kusimamisha uchaguzi, vema kwake kama angekuwa
amewasilisha hoja zinazosisitiza utetezi ili arejeshwe kugombea. Mimi si kamati
na wala sioni kama kuna ubaya kama Wambura akishinda kwa hoja kwa mujibu wa
kanuni na mwisho arejee kugomeba, halafu wanachama waamue.
Lakini si yeye awe kati ya wanaosisitiza uchaguzi
kusimamishwa! Hii ni ajabu kabisa, kweli anaona hilo ni sahihi, kweli ni sahihi
Simba wote waingie kwenye maumivu kwa kuwa mtu fulani hataki kukosa kitu fulani.
Kitu kingine naona kuna ujanja hapa, kwa kuwa Malinzi
ameona Wanasimba wamecharuka kuhusiana na kutaka uchaguzi uahirishwe, sasa
anataka apitie njia ya mkato ili baadaye aseme kamati ya rufaa ndiyo ilisimamisha
uchaguzi huo, hivyo si TFF, mimi nasema ujanja huu si sahihi na
umeishagundulika mapema.
Watu wa kamati hiyo si wale ambao wanajulikana kwenye
mpira kwa kiasi kikubwa, wanaweza kuamua kufanya lolote bila ya hofu ya lawama.
Lakini Malinzi anajua hawezi kufanya hivyo kwa kuwa Wanasimba wamempinga mapema
tu baada ya kuona alichosema si sahihi.
Hata kama mnataka madaraka kwa udi na uvumba, basi vizuri
muwe waungwana, ipeni Simba nafasi katika mioyo yenu na muamini inahitaji
maendeleo kwa kuwa wanachama na mashabiki wake wengi ambao ni wavumilivu, wameteseka vya kutosha bila ya
sababu za msingi.
Wakati mwingine naanza kufikiri kuna ujanja, kuna namna ya
kulazimisha kuwa ni lazima fulani awe kiongozi hata kama kuna makosa katika
njia yake kupita kwenda kuwania. TFF lazima muwe makini la sivyo mtachafuka
katika hili, toeni mikono yenu, acheni mambo yafuate utaratibu sahihi, Simba
isiwe sehemu ya kulipana fadhila.
0 COMMENTS:
Post a Comment