WAKATI watu wanasubiri kwa hamu burudani ya michuano
ya Kombe la Dunia inayoanza kesho, mamilioni ya fedha yatakayotumika
yanaonyesha kiasi gani inastahili kuwa michuano maarufu zaidi ya soka duniani.
Kombe la Dunia, kila nchi inataka kushiriki. Kwa hali
ya kawaida inajulikana ni njia ya kusaka heshima, lakini bado kuna kitu
kimejificha ndani yake.
Heshima kwa ajili ya rekodi za nchi, sawa. Lakini
mamilioni ya fedha yanayopatikana katika michuano hiyo yanaivuta nchi yoyote
kutaka kupata nafasi ya kushiriki.
Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) ambalo ni
mmiliki wa michuano hiyo limetangaza kuongeza mamilioni ya dola katika michuano
ya 2014 ukilinganisha na ile ya miaka minne iliyopita nchini Afrika Kusini.
Zaidi ya dola biloni moja, zitatumika ukijumlisha za
zile za kukamilisha maandalizi.
Lakini fedha za zawadi pekee kwa michuano ya Brazil
2014 ni dola 576, ikiwa ni ongezeko la asilimia 37 kwa upande wa zawadi.
Fedha hizo zinajumlisha kitita cha dola milioni 70
ambazo watalipwa timu za Brazil kama ambavyo umekuwa ni utaratibu wa Fifa
kuzilipa timu za sehemu husika inapofanyika michuano hiyo.
Lakini usisahau, timu zote 32 zinazoshiriki michuano
hiyo, kila moja tayari imelamba kitita cha dola milioni 1.5 kwa ajili ya
maandalizi.
Si kwamba baada ya maandalizi, timu hizo zitasubiri
kupata ushindi ili kupata zawadi nyingine ya milioni ya shilingi, kila hatua
ina malipo yake.
Kuhakikisha kama kweli michuano hiyo ni ya noti kweli,
kila timu itakayotolewa katika hatua ya makundi, kabla ya kuondoka, inaangwa na
kitita cha dola milioni 8.
Baada ya hapo, mbili kila kundi zinafuzu hatua ya 16
Bora, zile zitakazotolewa katika hatua hiyo, kila moja itaondoka na fungu la
dola milioni 9.
Fedha haziishii hapo, bado kuna zawadi ya wale
wanaotolewa inakuwa inaendelea. Utaona hapa kuna tofauti kubwa, kwani kila
anayetolewa, anatuzwa. Wao Fifa wanasema ni fedha za shukurani kwa ushiriki kwa
yule aliyetolewa.
Timu ikitolewa hatua ya robo fainali, nayo inalamba
dola milioni 14. Maana yake kila timu inayosonga mbele, haipati kitu lakini
inazidi kusogea kwenye mamilioni kwa wingi zaidi.
Maana yake sasa ni hatua ya nusu fainali na hapo ndiyo
kufuru ya fedha za Fifa inaanza kuonekana kwa kuwa timu zinakuwa zimebaki nne
tu.
Itakayoshika nafasi ya nne inapata dola milioni 20 na
dola milioni 22 zinatolewa kwa anayepata nafasi ya tatu.
Zinabaki timu mbili ambazo unazungumzia fainali, wengi
hapa akili inakuwa ni katika kombe maarufu zaidi katika soka kwa kuwa kulitwaa
ni heshima kubwa.
Lakini bado kuna fedha nyingi zaidi, timu
itakayopoteza katika fainali inashika nafasi ya pili na kupata dola milioni 25
wakati bingwa anaongezewa milioni 10 zaidi.
Dola milioni 35 kwa bingwa si kiduchu, fedha ambazo
zingeweza kuendesha soka ya Tanzania kwa zaidi ya miaka mitatu kwa mafanikio na
mabadiliko makubwa.
Hivyo usione wanaume wanapambana uwanjani ukadhani
wamejenga kupata heshima au ujiko pekee, noti noti pia ni nguvu nyuma ya
msukumo wa ushindi.
0 COMMENTS:
Post a Comment