SULLEY Muntari anaaminika ni kati ya watu wastaarabu na wenye
huruma sana nchini Ghana, hilo amekuwa akilithibitisha kwa vitendo.
Mfano mzuri ni saa chache zilizopita pale kiungo huyo nyota
wa AC Milan ya Italia alipoamua kwenda kutoa msaada kwa watoto maskini kabisa
nchini Brazil.
Kwa ruhusa ya kocha wake, Kwesi Appiah, Muntari alikwenda
kuwatembelea watoto wa eneo la Maceio ambao ni kati ya maskini zaidi duniani.
Akiwa hapo, pamoja na kuzungumza na kupiga nao picha, aliamua
kuwapa fedha kwa ajili ya mahitaji yao muhimu.
Huruma ya Muntari ni ya kibinadamu, lakini anaaminika ni mmoja
wa viungo wachache wakatili zaidi linapofikia suala la kupiga mashuti, hawaonei
huruma makipa.
Mfano wa mashuti hayo, moja alipiga katika mechi ya Kombe la
Dunia hatua ya makundi wakati Ghana ilipokuwa inapambana na ‘wagumu’ Ujerumani.
Shuti lake lilikuwa gumzo lakini kwa umahiri wa kipa Manuel
Neuer ambaye ni mmoja wa makipa bora duniani, aliweza kuliokoa.
Pamoja na mashuti, Muntari ameweka rekodi ya kuwa mchezaji
aliyepiga pasi nyingi ndefu na zikafika. Alipiga 16, zikafika 12, ikiwa ni
rekodi ya ‘jicho la mbali’ au maarufu kama jicho la mwewe.
Kitaalamu, uwezo wa kupiga pasi nyingi za mbali ni kipaji
ambacho wamebarikiwa wachezaji wachache sana. Mmojawao ni Muntari.
Pamoja na pasi hizo, Muntari anaweza kuwa mfano wa wachezaji
wengi ambao wakikaribia au kufikisha miaka 30 hujiona wamezeeka. Yeye katika
miaka 29 amekuwa ndiye nyota wa timu, tegemeo na sasa Ghana wanajiuliza mara
mbili kukosekana kwake katika mechi ya mwisho dhidi ya Ureno itakuwaje, maana
ana kadi mbili za njano.
Wachezaji wengi wa nchini wamekatishwa tamaa mapema, miaka 27
anaanza kuonekana mzee, anaitwa mzee, naye anakubali na ndiyo unakuwa mwisho wa
mpira wake.
Lakini katika
umri huo, Muntari kama ndiyo anaanza, tegemeo la kuchezesha timu, mashambulizi
yote ya Ghana dhidi ya Marekani na Ujerumani yalikuwa yakianzia kwake.
Hata Kocha wa Ujerumani, Joachim Loew alisema ingekuwa rahisi
kuimaliza Ghana kwa kumzuia Muntari kutocheza katika kiwango chake, lakini
halikuwa jambo rahisi.
Kingine ambacho kinaweza kuwa tofauti na wachezaji wa hapa
nyumbani, kwa umri wa miaka 29, tayari Muntari ana michuano mitano ya Kombe la
Dunia.
Kombe la Dunia kwa timu za taifa mara nne, akianza na ile ya
mwaka 2001 kwa vijana chini ya miaka 21, alicheza mechi saba na akiwa na Ghana
ikashinda mechi tano.
Kwenye Kombe la Dunia la klabu, mwaka 2010 akiwa na Inter
Milan chini ya Jose Mourinho wakalibeba.
Kwa timu kubwa za taifa, ameshiriki makombe matatu ya dunia
akianza na Ujerumani 2006, Afrika Kusini 2010 na sasa yuko anapambana nchini
Brazil.
Hiyo inamfanya azidi kuwa bora kwa kuwa ana nafasi ya
kushiriki michuano mikubwa tokea akiwa kinda, kitu ambacho wachezaji wengi wa
nyumbani hawapati, hali inayowapunguzia kujiamini.
Kwa uchezaji wa Muntari, anaweza kuendelea kung’ara kwa miaka
mingine mitano na huenda akacheza tena Kombe la Dunia 2018 nchini Urusi.
Wachezaji kama yeye, wanaweza kuwa funzo kubwa kwa wachezaji
wa hapa nyumbani. Kama wakipata nafasi wanaweza kurudia kuangalia mechi kati ya
Ghana na Ujerumani, namna Muntari alivyokuwa tatizo kubwa kwa Wajerumani huku
Sami Khedira na Toni Kroos wakiteseka.
Wajerumani waonasifika kwa ugumu, nguvu, kasi na pumzi ya
kutosha lakini kupitia pasi zake, ufundi na utundi wake walichemsha, wakatoka
kwa bahati tu!
0 COMMENTS:
Post a Comment