UKIWA muoga
katika nchi hii hasa katika masuala ya soka, basi utaishi umefunga mdomo milele
kwa lengo moja tu, kila mtu anataka umfurahishe yeye.
Si rahisi
kumfurahisha kila mmoja lakini si vizuri kufanya kazi hasa ya kitaaluma kwa
ajili ya kuwafurahisha watu. Kama unapenda hivyo, vizuri kuwa mwanamuziki au
muigizaji kwa kuwa wanaigiza fedha kwa ajili ya kufurahisha watu.
Soka ya
Tanzania imejaa wanafiki wengi, watu wanaoangalia maslahi yao na wanaochukia
wanaosema ukweli. Mifano iko mingi sana lakini huenda kunaanza kuibuka vijana
wadogo wanaotoa masomo na sasa yanapaswa kufuatwa na watu wazima.
Hivi
karibuni washambuliaji wawili wa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
(DR Congo), Mbwana Samatta na mshikaji wake, Thomas Ulimwengu waliamua kupanda
ndege hadi mkoani Mwanza kwenda kumjulia hali kocha msaidizi wa zamani wa Taifa
Stars, Slyvestre Marsh.
Marsh
amekuwa mgonjwa kwa zaidi ya miezi mitano sasa, alisafirishwa hadi jijini Dar
es Salaam kwa ajili ya kupata matibabu, lakini baadaye amerejea Mwanza ambako
anaendelea kupata matibabu.
Kabla ya
hapo, kulikuwa na hali ya kumtelekeza, gazeti hili la Championi likafuatilia,
likaandika na picha zikapigwa waandishi wake wakiwa wodini na Marsh, ilikuwa
kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Marsh
alikuwa amelazwa kwenye wodi ya kawaida, Championi likaeleza mazingira
ukizingatia yeye alikuwa mwalimu wa Taifa Stars. Siku chache baadaye, TFF
ikaibuka na kufafanua jambo hilo, huku ikisisitiza aliletwa Dar es Salaam na rais
wa shirikisho hilo.
Lakini
haikufafanua wodi anayokaa, haikufafanua vipi hakukuwa na kiongozi aliyefika
pale hospitalini kwa zaidi ya siku nne na hata rais wao pia hakuwa amefika!
Lakini mwisho, akahamishwa wodi na matibabu yake yakaanza kufuatiliwa kwa
ukaribu kabisa.
Baada ya
Marsh kurudishwa nyumbani kwake Mwanza, tunarudi nyuma kama Championi
lilivyoandika. Nani tena aliwahi kwenda kumjulia hali au kufuatilia kwa ukaribu
kinachoendelea? Jibu hakuna.
Lakini
Samatta na Ulimwengu wameonyesha uungwana ambao sasa unawagusa wengi, unaweza
kuliita darasa na watu hata wale wanaowazidi umri wanapaswa kujifunza kupitia
vijana hao.
Marsh yuko
Mwanza, wao wanafanya kazi DR Congo. Lakini baada ya kufika nchini wamefanya
safari ya kwenda katika jiji hilo la pili kwa ukubwa kwenda kumuona kocha wao
tena Ulimwengu akasisitiza kuwa Marsh alikuwa akimpa mazoezi peke yake ili
kuhakikisha anakuwa fiti.
Wachezaji wa
Mwanza mlifika kumuona Marsh, kwa mliofanya hivyo huo ni uungwana. Ambao
hamjafanya hivyo mtafakari, lakini je, wachezaji wengine wa Taifa Stars ambao
mlifanya kazi na Marsh ambao mnaishi hapa nchini mmewahi kwenda kumsalimia au
kumpa pole?
Kama haujafanya
basi lazima ujifunze kwamba Samatta na Ulimwengu, licha ya kuwa na mafanikio,
mfano hivi; majina makubwa, wanalipwa fedha nyingi kuliko wachezaji karibu wote
wa hapa nchini, lakini bado wamekumbuka suala la ubinadamu.
Vipi wewe
ambaye jina lako halina ukubwa kama la kwao, usiye na mshahara mzuri kama wao,
lakini bado haukumbuki mateso ya mwalimu wako au mtu uliyewahi kufanya naye
kazi.
Ubinadamu ni
msingi, hata uwe na uwezo wa vitu vingi sana, ubinadamu unabaki kuwa muongozo
wa mambo mengi sana ya msingi na moja ni kama hilo la Marsh ambalo ni mfano na
funzo, shule ambayo haina ada lakini ukijifunza utahitimu na kupata cheti
kitakachokusaidia mbele.
Hongereni
Samatta, Ulimwengu. Wengine liwe somo.
0 COMMENTS:
Post a Comment