June 21, 2014



Na Saleh Ally
KAMATI ya rufaa ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imepitisha uamuzi kuwa aliyekuwa mgombea wa Simba katika nafasi ya urais, Michael Richard Wambura kweli alifanya kosa.
Kosa la Wambura halijabadilika kama ambavyo kamati ya uchaguzi ya Simba ilivyoamua kwamba alifanya kampeni kabla ya wakati uliopangwa.


Vieleleza vilivyotolewa na kamati ya uchaguzi ya Simba vilikuwa wazi, imara na mwisho kamati ya rufaa ya TFF ikaona kila kitu kilikuwa ni sahihi hivyo ikapigilia msumari kwamba Wambura.
Sifa ya Wambura ni ubishi, kwamba huwa hakubali, hivyo matarajio ya wengi anaweza akafanya jambo, anaweza akakata rufaa tena au kuna watu wanaomuunga mkono wanaweza kuamua kwenda mahakamani.
Watu wanaomuunga mkono wanaweza kufanya hivyo, iwe kwa shinikizo lake au wao wenyewe kwa mapendekezo yao tu kutokana na mapenzi yao kwa Wambura hivyo wakaamua kufanya lolote.
Jana katika Hoja Yangu nilizungumzia kuhusiana na hoja tisa alizowasilisha Wambura kwenye kamati ya rufaa ya TFF. Kati ya hizo, moja ilikuwa inasisitiza uchaguzi wa Simba kusimamishwa kama alivyosema Rais wa TFF, Jamal Malinzi.
Nilipinga hilo, sikuona kama ilikuwa sahihi Wambura  kumuunga mkono Malinzi ambaye alifikia uamuzi mgumu kama ule bila ya kamati ya utendaji ya TFF kukutana na kujadili.
Yeye mwenyewe kuamua jambo kubwa kama hilo, haikuwa sahihi. Lakini hata Wambura kutaka uchaguzi usimame kwa maana ya maslahi ya Simba, bado si sahihi.
Amejaribu njia zote, maana yake hivi, kamati ya uchaguzi ya Simba imeona ana makosa mara mbili. Kamati ya rufaa ya TFF imeona ana makosa mara moja kwa kuwa mara ya kwanza ilimrudisha kwa kura za vidole na safari hii imepitisha kisheria kuwa ana makosa.
Kutoka Simba imeonekana ana makosa, kutoka TFF pia ameonekana ana makosa. Hivyo ni wakati mwafaka kwake kuona haitakuwa hivihivi, basi atafakari na kuanza kuangalia kila alipoambiwa kuna tatizo, apafanyie kazi.
Umri wa Wambura bado unamruhusu akiamua kuingoza Simba, ninachosisitiza ni hivi aanze kuzifanyia kazi dosari alizoelekezewa mara moja na kujipanga kwa uchaguzi mwingine lakini si kuendeleza malumbano zaidi.
Simba inahitaji umoja, inahitaji umoja wa Friends of Simba, Wambura, wanachama wengine, mashabiki na wadau wake ili kufanya mambo vizuri ili kuirejesha katika hali nzuri.
Kunapokuwa na umoja ni lahisi mambo mengi kwenda haraka, lakini kama kikundi kimoja mtakuwa mnapambana baina yenu, basi itakuwa ni kazi ngumu sana maendeleo kupatikana.
Simba hadi sasa wanajua wanamhitaji nani awe kiongozi. Kama itatokea rais mpya amepatikana na si Wambura basi litakuwa jambo la msingi kwa Wambura kumpa ushirikiano kiongozi huyo mpya.
Lakini itakuwa vizuri zaidi kiongozi huyo mpya kumshirikisha Wambura katika mambo ya klabu hiyo katika kipindi ambacho anarekebisha mambo yake ili awe mwanachama asiye na walakini na ikifikia kutaka kugombea, asiingie kwenye vikwazo tena.
Simba inahitaji Wanasimba ili kufanya vizuri, makundi hayawezi kuisaidia klabu hiyo ambayo imekaa ‘vibaya’ katika kipindi hiki kurudi katika sifa kubwa iliyokuwa nayo mwanzoni mwa miaka ya 1990 na 2000.
Hakuna ujanja, hata kama malaika wa Baraka atashuka ndani ya klabu hiyo, au rais mpya akawa ni mtu mwenye uwezo mkubwa wa kufikiri na kutafakari. Lakini kama hakuna umoja baina yao, hadithi itakuwa ileile na kila mmoja ataishia kumcheka mwenzake huku Simba ikizidi kupotea.
Ndiyo maana nikasisitiza kwa Wambura, kwamba sasa si muda wa rufaa wala mahakama. Badala yake kipindi kizuri cha kuangalia maisha ya Simba ambayo imekuwa ikiishi shimoni kwa kipindi chote cha miaka minne iliyooita ya ‘rafiki yangu’ Ismail Aden Rage.
Simba inawahitaji Wanasimba kufanya kazi kwa ushirikiano wa hali ya juu kwa ajili ya maendeleo yake ambayo ndiyo maendeleo ya Wanasimba. Badilikeni, zungumzeni na unganeni, malumbano na chuki ndiyo yaliyowafikisha hapo, yaepukeni.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic