NAJUA ulipata taarifa kwamba Mwenyekiti wa
Yanga, Yusuf Mehbub Manji aliandika barua kwenda kwa rais mpya wa Simba, Evans
Aveva.
Barua ya Manji kwenda kwa Aveva ilikuwa ni
kumpa pongezi kutokana na kufanikiwa kwake kutwaa uongozi wa Simba.
Pongezi na kumkaribisha kwenye mbio za
kuendeleza soka na inaelezwa Manji alisisitiza yuko tayari kupambana na Simba
uwanjani, pia kushirikiana na Aveva na timu yake ya uongozi kusaidia kupatikana
maendeleo makubwa kwa klabu hizo mbili kongwe.
Yanga na Simba, iwapo zitatokea zikavurunda,
basi kwa kiasi kikubwa zinachangia kuyumba kwa soka hapa nchini kutokana na
nguvu zao na sapoti kubwa kutoka kwa wanachama na mashabiki wake.
Siku hizi wameibuka baadhi ya viongozi wa
Azam FC ambao wanakasirishwa eti kwa kuwa stori zao hazijatumika na kuwa kubwa
kama zile za Yanga au Simba, wakiamini sasa ni wakubwa sana, kitu ambacho
kinaonyesha kiasi gani hawajui walipo.
Hakuna ubishi Yanga na Simba, zimebeba
sehemu kubwa ya mpira wa Tanzania lakini zimekuwa zikishindwa kusonga mbele au
kufanya vizuri zaidi kutokana na ukosefu wa mambo mengi sana.
Kwanza hazishirikiani, pili watu wake
wamejengewa uzio, kila upande unataka uishi peke yake na zimekuwa ni timu za
rangi, eti Yanga wakimuona aliyevaa nyekundu anakuwa adui, hali kadhalika kwa
Simba na njano.
Wakati wa enzi za miaka ya 1930, 1940 hadi
1970, Simba na Yanga walikuwa ndugu nje ya uwanja, ndiyo maana akifariki mtu
ambaye ni mwanachama wa Simba, basi Yanga ndiyo walikuwa wanafanya kazi zote
msibani huku wakiwasihi wafiwa kukaa pembeni.
Hilo lilikuwa ni kuthibitisha kuwa kweli
Yanga na Simba ni watani wa jadi, lakini sasa sivyo, Simba na Yanga ni maadui
wa jadi na wale wanaoabudu rangi za njano na nyekundu, mimi nawaita mashabiki
na wanachama wa rangirangi, maana hawajui lolote.
Manji ameamua kumuandikia barua kumpongeza
Aveva, huo utakuwa ni mwanzo mpya wa wale rangirangi kuanza kutafakari kama
mwenyekiti wa klabu hiyo anaweza kufanya hivyo, basi wajifunze, wang’amue kuwa
ushindani wa timu hizo kama alivyoeleza Manji, utakuwa uwanjani na kupambana
kila sehemu.
Halafu Yanga na Simba, zinaweza kuwa na
nafasi ya kuunganisha nguvu sehemu, mfano katika kusaka wadhamini au kugombea
maslahi yao kwa kuwa wakati mwingine hazipati hadhi inayostahili na imefikia
hata zinaanza kulinganishwa na timu ambazo zisipocheza dhidi ya timu hizo
kongwe, haziwezi kuingiza hata Sh 500,000, kitu ambacho si haki pia ni
kuzinyonya.
Msijisikie vibaya kumpongeza Manji,
ameonyesha ni mtu ambaye ana lengo zuri na anapaswa kuungwa mkono. Anataka
kusaidia kuziondoa klabu hizo kongwe kwenye uongozi wa kizamani uliojaa
ushabiki usiokuwa na manufaa na kuangalia maslahi ya klabu hizo.
Ninaamini kwa Aveva, hakuna shaka, si wale
viongozi wa kizamani ambao wanataka kujali matumbo yao bila kuangalia klabu
inafaidika nini na kipi ni mafanikio.
Vizuri uamuzi wa Manji kutuma barua kwa
Aveva na Aveva kuipokea barua ya Manji ichukuliwe kama changamoto na kuanza
upya kwa karne ya Yanga na Simba zenye jicho linaloona mbali kama lile la
mwewe.
Yanga na Simba wa rangirangi, muda wao
umekwisha kwa kuwa wamezidumaza klabu hizo. Sasa ushirikiano kwenye maslahi ya
klabu, iwe inawezekana lakini kushindana uwanjani, iwe kama kawa.
Wale wazee wa zamani ambao wana mifano
mizuri kama kuzijengea klabu hizo majengo, ndiyo walikuwa wakifanya hivyo,
yaani kushirikiana. Mlipoingia nyie rangirangi, mkachangia klabu hizo kuanza
kudumaa.
Sasa ni Aveva na Manji na huu ndiyo wakati
mwafaka wa kuanza upya na kasi ya maendeleo ianze kupigwa, Yanga na Simba ni
tajiri lakini hazikuwa zimepata wanaoangalia mbali. Tafadhali, Manji, Aveva,
endeleeni kuinua vichwa.
0 COMMENTS:
Post a Comment