Na Saleh
Ally
MASHABIKI
wa Brazil waliamua kwenda uwanjani na vitu vingi kama ujumbe wa kutaka
marekebisho ya timu yao wakati wa mchezo wa mshindi wa tatu ambao waliamini
lazima watafungwa, lakini wakaamua kufanya jambo moja kama msaada.
Waliamini
msaada wao wa kuizomea kupindukia Uholanzi ungesaidia kuichanganya ili ifungwe
na Brazil, walikuwa hawana ubishi kuwa Brazil ilikuwa katika kiwango ambacho
hakilingani na ubora wa Waholanzi.
Hilo
halikuwa na ubishi, walifanya hivyo lakini timu ikaambulia kipigo kingine
kikiwa cha pili mfululizo, Waholanzi wakashinda 3-0 na kushika nafasi ya tatu.
Maana yake katika mechi mbili au dakika 180, Brazil ikawa imeruhusu mabao 10!
Ujumbe
walioingia nao uwanjani ulikuwa ni wa kila aina, lakini baadhi ya mabango
yalikuwa ni kusisitiza kuwa wamechoka kunyanyaswa na waliona bora mshambuliaji
wa zamani nyota zaidi dunia, Edison Arantes do Nascmento maarufu kama Pele
arudi.
Mashabiki
hao wanataka Pele arudi na kuiokoa Brazil, wengine wakaingia uwanjani na akina
mama waliokuwa wajawazito, wakionyesha kuwa Pele mpya au mwokozi wa Brazil
kuondoa manyanyaso yanayowakuta atazaliwa hivi karibuni.
Mashabiki
hao wa Brazil si wendawazimu, wanajua wanachokifanya na kwamba wanamhitaji Pele
arudi na kuanza kucheza, hataweza. Au arejee na kuwa kiongozi wa soka au kocha,
wanajua haitawezekana, wanalia wanahitaji mkombozi.
Wabrazili
wanaamini nchi hiyo ina wachezaji wengi walio na uwezo wa kucheza soka katika
kiwango cha kizazi cha kina Pele na Garincha au kabla ya hapo akina Didi, Vava
au baadaye wachezaji kama Socrates na hadi kufikia akina Zico, Romario, Bebeto,
Ronaldo na Ronaldinho.
Katika
michuano ya Kombe la Dunia mwaka huu, Brazil ndiyo timu mwenyeji ambayo ina
sifa ya kuwa bora zaidi katika soka katika kipindi kirefu na ndiyo inaongoza
kwa kulitwaa kombe hilo mara tano.
Mashabiki
wengi walikuwa na matarajio safari hii, kikosi ndiyo kilikuwa kinabeba kombe
hilo kwa mara ya sita na kuongeza rekodi yake ya kulichukua, lakini imekuwa
tofauti, aibu imetawala.
Brazil
ndiyo timu iliyobeba rekodi zote za kuumiza, kwanza kama wenyeji wamefungwa
mabao mengi zaidi kuliko timu yoyote. 7-1 dhidi ya Ujerumani, imeivuka ile 5-1
waliyofungwa waliokuwa mabingwa watetezi dhidi ya Uholanzi.
Katika
mechi saba walizocheza, wameruhusu mabao 13 wakati wao walifunga tisa, maana
yake ndiyo timu iliyokuwa na safu nyanya zaidi ya ulinzi kuliko nyingine zote,
inaonekana kubeba aibu ya Hispania ambayo iliondoka imefunga mabao manne na
kufungwa saba.
Rekodi ya
kufungwa mabao mengi zaidi kwenye nusu fainali ya Kombe la Dunia tangu mwaka
1930, sasa wanayo Brazil. Usisahau kama ni mabeki wa kati, basi Brazil inao
wawili, Thiago Silva na David Luiz ambao ni kati ya wale bora duniani.
Luiz ndiye
beki ghali zaidi duniani kutokana na uhamisho wake wa kitita cha euro milioni
42 (Sh bilioni 92) kutoka Chelsea kwenda PSG ya Ufaransa, lakini wameondoka
kwenye michuano hiyo wakiwa uchochoro.
Pamoja na
yote hayo, kocha Fellipe Scolari amesisitiza hatajiuzulu, huenda likawa kosa la
milele kama Brazil watamruhusu abaki na kuendelea kuinoa timu hiyo. Huu ni wakati
mwafaka wa Big Fill kufungasha virago na kuacha mawazo mapya ya Wabrazili
wengine kufanya kazi.
Pele
mwingine huenda akawa ameishazaliwa, Neymar pekee hatoshi, hivyo ni wakati
mwingine mzuri kwa Brazil kutoa nafasi kwa wanaoweza kuisaidia miaka minne
ijayo, la sivyo aibu itaendelea na mwisho taifa hilo litaondoka kwenye heshima
ya ubora wa soka waliyoaicha akina Pele.
Ndiyo maana
wengi wanalia, wanamhitaji Pele arudi, bado angerudi tatizo lisingekwisha kwa
kuwa Brazil iliyoshiriki michuano ya Kombe la Dunia nyumbani, iliingia na
makinda wengi bila ya wazoefu.
Scolari
ameambiwa, lakini amekataa ingawa ukweli ni kwamba, idadi ya wazoefu na vijana
haikulingana, aliamua kuamini vijana zaidi ambao hata kihesabu katika michuano
iliyoisha, hawakutamba sana kama wakongwe.
Kingine
kilichomuangusha Scolari, kikosi chake hakikuwa na washambuliaji viwembe kama
enzi za kina Ronaldo. Kina Fred na Jo, walikuwa ‘wanambwela’ tu!
0 COMMENTS:
Post a Comment