July 11, 2014




SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limetangaza kusogezwa kwa Ligi Kuu Bara hadi Septemba 20, huu itakuwa ni muda wa mwezi mzima kutoka kipindi kilichopangwa awali cha Agosti 24.


Timu nyingi zilikuwa zimeanza maandalizi kwa ajili ya Ligi Kuu Bara na lengo lilikuwa ni kuanza vizuri, hivyo maandalizi zaidi yalilenga Agosti 24 kama ambavyo TFF ilitangaza.

Uamuzi wa TFF kusogeza ligi hiyo hauna maelezo mengi sana, kikubwa ambacho kimeelezwa kwenye barua zilizotumwa kwenye klabu ni pamoja na kuipisha michuano ya Kombe la Kagame itakayofanyika nchini Rwanda.

Michuano ya Kagame imepangwa kuanza Agosti 9 hadi 23, yaani ingekuwa ni siku moja tu kabla ya kuanza kwa ligi kuu. Hivyo, TFF imeamua kusogeza mwezi mzima mbele, unawaelewa vizuri?

Timu za Bara zitakazoshiriki michuano hiyo ni Yanga na Azam FC, ili ziende hadi Agosti 23 lazima ziingie nusu fainali ili zicheze mechi ya mshindi wa tatu itakayokuwa Agosti 22 au fainali Agosti 23.

Kama timu ni mbili zinazoshiriki michuano hiyo, vipi zisogeze mbele ligi yenye timu 14? Maana yake 12 zote zinalazimika kusubiri. Maana yake hata kama zitatolewa baada ya siku tano, yaani hatua ya kwanza, bado ligi itaendelea kusubiri kwa mwezi mzima.

Ninacholenga ni kusema TFF inaonyesha haiko makini na huenda huu unaweza ukawa ni mwanzo wa kuanza kuboronga mambo mengi, inaonyesha huu ni mwanzo wa marudio ya ratiba ile ya kupakiwa viraka kila namna.

Unakumbuka Chama cha Soka Tanzania (Fat) na ile TFF ya mwanzomwanzo ambayo kila mara ratiba ya ligi kuu ilikuwa inapachikwa viraka kila kukicha na kila wanapojisikia kufanya hivyo?

Angalau TFF wakati wa Leodegar Tenga wakaonyesha kujitahidi na taratibu wakabadili mambo na upanguaji wa ratiba ulipungua kwa asilimia 90. Sasa TFF hii chini ya Jamal Malinzi imeanza upya kabisa, inasimamisha ligi kwa mwezi mzima bila sababu za msingi.

TFF imeamua kusimamisha ligi kwa kutuma tu barua kwenye klabu, hakuna kushauriana, haikukaa pamoja na klabu na kushauriana nazo na kueleza sababu ya msingi na mengine mengi.

Huenda Yanga au Azam FC wangeweza kusema wanapeleka timu B, hivyo ingekuwa rahisi TFF kuahirisha uamuzi wake wa kusogeza ligi kwa mwezi mzima. Pia wangeweza kusogeza ligi kwa wiki mbili pekee.

Klabu zina wadhamini ambao lazima watakuwa wana mipango na hao wanaowadhamini, inawezekana wadhamini hao wakawa wameanza maandalizi ya jambo fulani kwa ajili ya klabu wanazozidhamini.

Klabu ndizo zinazofanya ligi hiyo iwepo, TFF inapaswa kuonyesha nidhamu kwao badala ya kupeleka mambo kama mzazi dikteta ndani ya familia ambaye hajali ushauri na anafanya mambo yake anavyotaka bila ya ushauri wa vijana ambao ni wanafamilia pia.

Inawezekana washauri wengi ambao wamekuwa wakijulikana kama watu wa karibu na uongozi wa TFF pia wamekuwa ni tatizo, watu ambao wanaweza kuzungumza lolote na likapitishwa na raia wao bila ya kushauriana na watu wa ufundi.

Kuna kila sababu TFF kubadili mambo, waanze kuamini wao ni viongozi lakini timu kupitia uongozi wa klabu ndizo zinafanya uwepo wa ligi hiyo na zinapofanya mambo kwa uhakika, wadhamini wanakuwa tayari kuungana na kuzisaidia udhamini ambao unazipunguzia gharama.

Kuendesha mambo kwa kuwa kiongozi wa juu wa TFF au kundi la watu fulani limeamua kufanya na inafanyika tu, haitakuwa sawa na ndiyo utakuwa mwanzo wa kuonyesha uongozi wa TFF chini ya Malinzi umefeli mapema!

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic