July 21, 2014

RAIS WA TFF, JAMAL MALINZI


Na Saleh Ally
MAMA mzazi wa mshambuliaji nyota wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo, aliangua kilio cha uchungu wakati akielezea namna alivyofanya zoezi la kutaka kuitoa mimba ya nyota huyo kutokana na ‘stresi’ za maisha.


Maria Dolores alisema alifanya juhudi za kuitoa mimba ya Ronaldo, lakini daktari akamkatalia katakata na kumueleza asingefanya kazi hiyo, aliondoka hospitali akiwa na hasira na kurejea nyumbani.

Alipofika kwake katika Mji wa Madeira nchini Ureno, aliamua kufanya juhudi za kuitoa mimba hiyo kivyake, kwanza alikunywa pombe kali ya moto, halafu akafanya mazoezi magumu sana na mwisho, akaenda kulala.

Alipoamka asubuhi, alitarajia kupata majibu ‘mazuri’ kama alivyotaka, lakini kilichomshangaza, bado alikuwa mjamzito, naye akakata tamaa na kukata shauri la kuzaa, mwisho akazaliwa Ronaldo, tegemeo la Real Madrid na Ureno.

Maisha yana mambo mengi sana, yanakuja na kupita lakini kujifunza ni vema, ndiyo maana nimeanza na kisa hicho cha mama Ronaldo kwa kuwa machozi yake yalikuwa yanadondoka na mafunzo kwa wengine.

Mungu yupo siku zote, ndiye kiongozi wa kila jambo hasa la kheri, lakini kila mmoja anatakiwa kuwa mwenye kufikiri na kutafakari, lakini kufanya mambo kwa uamuzi sahihi na si kutegemea kila anachoelezwa.

Mama yake Ronaldo, aliamua kuitoa mimba yake, lakini ndiye aliyeamua kutoitoa baada ya kushindwa kufanya hivyo. Hata akijuta leo, basi bado ana sehemu angalau ndogo ya kujipongeza kwa uamuzi wa mwisho wa kutoitoa.

Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi naye ni binadamu, ningependa nitumie mfano huo wa kuamua kufanya au kutofanya wa mama Ronaldo kuangalia mwenendo mzima wa TFF ambayo sasa inaonekana inakwenda pabaya.

Nimekuwa nikitafakari na kuona huenda Malinzi anaweza asiwe ‘mtu mbaya’ ambaye ana nia nzuri, lakini amezungukwa na wapambe, watu wengi ambao si sahihi na wanaomshauri kufanya mambo mengi kwa kukurupuka.

Angalia viingilio vikubwa vya mechi ya Taifa Stars dhidi ya Msumbiji kwa madai kwamba gharama ya maisha imepanda, niite hoja hiyo ni ya msingi. Lakini inaonekana wazi TFF inafanya hivyo ili kuweka mambo sawa kutokana na madeni au kuweka mambo vizuri.

Sitaki kusema nitaweka kipaumbele taarifa za wafanyakazi wa TFF kutokuwa wamelipwa mshahara, inawezekana walicheleweshewa kidogo tu kama siku 20 hivi, hivyo si jambo kubwa, lakini vipi kuhusu hawa mashabiki wa soka wanaotaka kuiona Taifa Stars?

Kichekesho kinatokea ukisikia TFF inawataka mashabiki kujitokeza kwa wingi kuishangilia timu yao wakati inapambana dhidi ya Msumbiji, halafu inaweka kiingilio kikubwa cha kuingia uwanjani, wakati kukiwa na taarifa za Azam TV kuonyesha mechi hiyo!

Angalia kama ni suala la washauri, ndiyo maana nasema ni watu wa kukurupuka, lakini kama kweli hili ameamua Malinzi mwenyewe, basi kichekesho kingine lakini bado anapaswa kupongezwa kwa uamuzi wake wa kujaribu kama alivyoamua jambo mama Ronaldo!

Kama kiingilio kikubwa, halafu watu wana uwezo wa kuiona mechi kwenye runinga, basi watabaki nyumbani au kwenye baa waangalie. Kama itaonyeshwa, vipi TFF isipunguze kiingilio ili watu wajitokeze kwa wingi kuipa nguvu timu yao? Unajua mashabiki nyumbani ni silaha ya mwenyeji.

TFF haiwezi kusema imetumia fedha nyingi za kuandaa timu, tunajua kuna mdhamini ambaye anafanya jukumu hilo naye angependa kuona mafanikio na hasa suala la ushindi na mashabiki wakiingia kwa wingi kuishangilia timu hiyo na ndiyo maana ya business benefits (faida za kibiashara).

Sijajua TFF imepata kiasi gani kuiuzia Azam TV matangazo ya kuonyesha mechi hiyo, fedha ni jambo muhimu, lakini mashabiki kuwa uwanjani kwa wingi ni jambo muhimu zaidi kwa kuwa timu ikisonga mbele, kunakuwa na nafasi ya kupata fedha zaidi na mafanikio zaidi kwa taifa.

Inashangaza zaidi ukiona eti hata waandishi wamezuiwa kuingia, sasa TFF imeamua waingie wawili tu kwa kila chombo, kwa kuwa washauri wamesema wanajaza uwanja, lakini TFF au Malinzi hawajawahi kulipia hata mara moja wanapoitisha mkutano au kusema wanataka mwandishi na mpiga picha tu.

Hii inaonyesha kweli TFF wanahitaji sana fedha, wameamua kukusanya hata za waandishi ili mradi mambo yakae sawa. Nikabaki najiuliza, ni kwa kuwa wanataka kulipa pango la kodi wanayodaiwa?

Usisahau TFF imehamia kwenye jengo la PPF Tower, Posta jijini Dar es Salaam, ikaacha ofisi zake nzuri kabisa kwa madai kunatakiwa kufanyika ujenzi wa uwanja na hosteli. Bado tunaendelea kuzisubiri na hizo Sh milioni 15 kwa mwezi wanazotoa kama kodi, zitaendelea kuongezeka tu.

Ukubwa wa kodi, huku TFF ikiwa haina vyanzo vikubwa vya mapato ni kutaka Malinzi aanze kuangusha mzigo kwa wananchi na waandishi, lengo kwake ni kutimiza mahitaji ya kifedha.

Najua Malinzi atapinga, wapambe pia wanaweza kung’aka, lakini huu ndiyo ukweli kwamba mapema sana, TFF chini ya Malinzi inapotea tena kwenye mambo mengi sana.

Mmoja wa wasomaji wa gazeti hili, alinipigia simu na kusema ataanza kuichukia Taifa Stars kwa ajili ya Malinzi. Leo namalizia hapa kwa kumjibu kuwa Taifa Stars ni yangu, yake huyo msomaji, yetu na asiichukie hata kidogo kwa kuwa si ya Malinzi wala hao washauri wake!




0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic