July 21, 2014


JAJA

Na Saleh Ally
NDANI ya Tanzania, Yanga si ya kwanza kuleta wachezaji kutoka Brazil, Malindi ya Zanzibar waliwahi kufanya hivyo katika miaka ya 1990 na 2000 mwanzoni.


Pamoja na hivyo, kipindi Malindi walicholeta Mbrazil, si hiki cha sasa ambacho kina mabadiliko makubwa na kwa Tanzania Bara, Yanga wamethubutu ikiwa ni msimu mmoja tu baada ya Coastal Union kumleta mchezaji kutoka Brazil, Gabriel Barbosa lakini siku chache akashindwa na kurejea kwao.

Safari hii Yanga wamekuja kivingine, wameajiri Wabrazil wanne na inaonekana wamepania kuingia kwenye mabadiliko kwa kuwa timu hiyo ya wageni ina jukumu la kuonyesha nini kipya.

Wabrazil hao ambao ni makocha wawili, Marcio Maximo, msaidizi wake Leonaldo Leiva na wachezaji, kiungo Andrey Coutinho na mshambuliaji Edielson Santana ‘Jaja’, watasaidiana na Waganda, Wanyarwanda na Watanzania kuitafutia Yanga mafanikio ya msimu wa 2014-15.

Si kazi rahisi ushindani wa msimu ujao na kinachoonekana watu wa Yanga watakuwa wamejaa matumaini makubwa sana na Jaja na Coutinho wakiamini Wabrazil ni watu wa soka hasa, hivyo hakuna kitakachoshindikana, hilo ni kosa.
 
COUTINHO
Soka la sasa limebadilika, kila sehemu wanaweza kuucheza mchezo huo ndiyo maana hata Azam FC ina kocha kutoka India na mafanikio yanapatikana kwenye timu za vijana.

Jaja na Coutinho hawawezi kuwa kila kitu, lakini wanaweza kuwa chanzo cha mabadiliko makubwa ya soka ya Tanzania kupitia watakachokifanya angalau kwa nusu msimu tu.

Majibu ya kuwa wachezaji wa Brazil wanaweza kuwa fundisho kwa soka ya Tanzania, hayawezi kupatikana katika mechi mbili au tatu, soka yetu ina utamaduni wake na aina ya uchezaji, ndiyo maana wachezaji hata kutoka nchi za jirani tu wamekuwa wakilalamika.


Mfano mzuri, Amissi Tambwe pamoja na kufunga mabao 19 na kuibuka mfungaji bora wa msimu, alilalama na kueleza ugumu wake akilinganisha na kwao Burundi. Jiulize Jaja na Coutinho, watauweza ‘mziki’ wa mabeki ‘vichwa ngumu’ wa Kibongo?

Kwa mechi 16 za mwanzo za msimu, Coutinho na Jaja watakuwa wametoa jibu kuwa kusajili Wabrazil au wachezaji wa Bara la Amerika Kusini katika soka ya Tanzania, itakuwa ni kusaidia kukuza uchanga wa soka yetu au ndiyo kupigwa changa la macho?

Wamekuja hapa na wameonyesha juhudi kubwa mazoezini, tayari hiyo inaweza kuwa tofauti kubwa na wachezaji ambao wamekuwa wakichota mamilioni ya Watanzania hasa wale wanaotokea Uganda na Kenya. Lakini pia kuna haya ya kujifunza.

Wamethubutu:
Bado Yanga wanapaswa kupongezwa kwa kuwa wamethubutu, huenda kila mtu tayari kaingia hofu na wapinzani wao wanasubiri kuwacheka kutokana na walichokifanya, hasa wakifeli.

Ikitokea wakafeli wataonekana kichekesho, lakini kama watafanikiwa, basi wataonekana ni mashujaa na inawezekana kuna klabu nyingine zitaamua kuimarisha vikosi vyao kwa kuchukua wachezaji kutoka Brazil, Argentina, Colombia, Chile au kwingineko.

Funzo:
Coutinho na Jaja wanaweza kuwa funzo si kwa Yanga tu, hata kwa timu nyingine zenye uwezo wa kununua wachezaji kutoka nje ya Brazil kama walikuwa wanatamani kufanya hivyo.

Mfano, wakifanikiwa jibu litakuwa ndiyo wafuate nao kutoka huko Amerika, wakifeli waachane nao na kuendelea na sehemu nyingine za Bara la Afrika.

Lakini wachezaji wa Brazil pamoja na mikiki ya ligi ya nyumbani, wanaviweza viwanja vya Kibongo, hasa vile vya mikoani ambavyo mchezaji anacheza huku anaruka kokoto.

Kila mchezaji anakimbia huku akihofia kuanguka. Angalia Coutinho alianguka mara moja tu pale Tandika, kovu kubwa. Itakuwaje ligi ikianza? Jibu ndiyo litakuwa mafunzo na mechi za mzunguko wa kwanza zitakuwa na jibu sahihi.

Jaja&Coutinho:
Wameanza kwa kuonyesha tofauti kutokana na juhudi mazoezini, lakini wameonyesha tofauti nyingine ya kuwa si watu wenye makuu baada ya kuomba waishi katika eneo la Kariakoo ambalo wachezaji kutoka Kenya, Uganda, Rwanda na kwingine wasingependa.

Wengi wamekuwa wakichagua Masaki, Osyterbay, Mikocheni, Sinza na kwingineko kwa kuwa ni sehemu wanayoishi watu wa daraja la juu au kati.

Kina Coutinho wameamua kujichanganya Uswahilini, katikati ya jiji na wanataka kukaa karibu na Klabu ya Yanga. Hayo ni mapenzi, kweli hawapendi makuu au ujanja wa kupoza makali kabla, kwamba hata wakifeli wasamehewe kuwa si wapenda makuu?

Tayari kuna mambo ya kuhifadhi ili kusubiri mafunzo kutokana na kitakachotokea, lakini inaonyesha shule kupitia Wabrazil hao imeanza.



Ushabiki:
Kila mmoja anataka kuona Wabrazil hao wanapata mafanikio na kufanya kazi yao, hilo ndilo bora kwa Yanga na mashabiki na wanachama wake.

Lakini kuna haja ya kupima mengi kwanza, kwamba Maximo alivyofanya vizuri na timu ya taifa, Taifa Stars kwa mechi chache, bila ya kucheza mikoani kwenye viwanja vibovu. Je, ataweza akiwa na Yanga inayokwenda kuivaa Ndanda ndani ya Nangwanda Sijaona kule Mtwara?

Viongozi, mashabiki na wanachama kuamini kwamba kwa Wabrazil hao, makocha na wachezaji kila kitu kitawezekana ni sahihi? Jibu litakuwa hapana na watakapokwama kwa wakati fulani, bado presha kubwa wakiachiwa itawamaliza kabisa na mwisho wataondoka mapema.

Kuwapa muda mwingi wa kufanya vizuri si sahihi, lakini kuwapa angalau muda fulani ni vema kwa kuwa wao pia wana vitu vya kujifunza ili wakae sawa, lakini moja kwa moja wakianza vizuri, basi itakuwa vizuri na itakuwa imejulikana watasaidia soka ya Tanzania kutoka kwenye uchanga kupanda juu au ujio wao watakuwa wameipiga Yanga changa!


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic