Hii ni hatari, utani wa miaka nenda rudi kati ya
timu kongwe nchini, Simba na Yanga, umeonekana kugeuka chuki na ukatili,
kufuatia kitendo cha mashabiki wa Simba kumvamia shabiki mmoja aliyesadikika
kuwa wa Yanga na kumvua jezi kisha kuichoma moto hadharani.
Akiwa amevaa jezi namba saba yenye jina la
Coutinho ambaye ni kiungo mpya Mbrazil wa Yanga, baadhi ya mashabiki wa Simba
waliokuwa wakifuatilia mazoezi ya timu yao, walimvamia, wakamvua jezi hiyo
kisha kuichoma moto.
Championi lilishuhudia shabiki wa Simba
akitokea akiwa ameshikilia jezi ya rangi ya njano na kijani huku akisaka kiberiti.
Hata hivyo, haikuchukua dakika mbili,
mashabiki walianza kupiga kelele, wakitafuta kiberiti, ndani ya dakika,
walichukua kiberiti na kuiteketeza na kuitundika mtini huku wakishangilia.
Wakizungumza na SALEHJEMBE kwa nyakati tofauti, mashabiki hao wa Simba,
wote kwa kauli moja walikuwa wakipinga kitendo cha jezi ya Yanga kuonekana
kwenye mazoezi yao.
“Kwani hapa ni Loyola mpaka aje na jezi ya
mkosi? Hapa ni Simba tu, kama vipi aje achukue hela akanunue nguo nyingine
lakini si jezi ya Yanga, kama amekosea njia, basi imeshakula kwale,” sauti
mbalimbali za mashabiki zilisikika wakati wakitekeleza ‘ukatili’ huo.
Wakati hayo yakiendelea, shabiki mwingine
aliyekuwa amevaa jezi kama hiyo, alitimua mbio baada ya kuona kitendo
kilichofanyika uwanjani hapo.
0 COMMENTS:
Post a Comment